Habari Mseto

Magavana sasa kusimamia uainishaji wa miji na manisipaa katika kaunti zao

March 13th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI za kaunti sasa zimepewa mamlaka ya kubadili vigezo vya kuainisha eneo fulani kama jiji, manispaa, mji au kituo cha kibiashara.

Hii ni baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutia saini Mswada wa Marekebisho ya Sheria kuhusu maeneo ya miji na Miji Mikuu, 2018 kuwa sheria.

Chini ya sheria hii mpya, idadi ya watu inayohitajika kwa mji kupandishwa hadhi kuwa jiji imebadilishwa kutoka watu 500,000 hadi 250,000.

Kando na kigezo cha idadi ya watu, mji ambao utachukuliwa kuwa jiji sharti udhihirishe kuwa na uwezo wa kuzalisha mapato ya kufadhili shughuli zake kando na kuwa na miundo msingi bora, mathalan barabara za kisasa.

Sheria hii mpya inairuhusu serikali za kaunti kutangaza mji kuwa manispaa ikiwa una angalau wakazi 50,000. Vilevile, eneo ambalo litaitwa mji sharti liwe na angalau wakazi 10,000 huku kituo cha kibiashara kikihitajika kuwa na angalau wakazi 2,000.

Aidha, sheria hiyo inapendekeza kuundwa kwa bodi maalum za kusimamia miji na manispaa kando na kuorodhesha mahitaji maalum ya watu ambao watateuliwa kusimamia bodi husika.

Sheria ya Maeneo ya Miji na Miji inawapa magavana wajibu wa kusimamia na kuendesha miji na manispaa na vituo vya kibiashara katika kaunti zao.

Manispaa

Wakati huu, ni miji miwili pekee nchini ambayo inaainishwa kama manispaa huku kukiwa na miji 130 kote nchini.

Rais Kenyatta pia alitia saini Mswada wa Mafuta ambao unapendekeza kuundwa kwa mashirika matatu ya serikali ya kusimamia na kushirikisha matumizi ya rasilimali ya kawi nchini. Mashirika haya ni Mamlaka ya Kusimamia Kawi na Mafuta, Shirika la Uwekaji Umeme Mashambani na Kawi Endelevu na Shirika la Kawi ya Kinuklia.