HabariSiasa

Magavana si vituo vya polisi kupewa walinzi 26 – Matiang'i

May 21st, 2018 1 min read

Na LEONARD ONYANGO

WAZIRI wa Usalama Fred Matiang’i Jumatatu ametetea uamuzi wake wa kuwapunguzia magavana walinzi huku akisisitiza kuwa serikali haitalegeza kamba.

Dkt Matiang’i aliyekuwa akizungumza jijini Nairobi alipopokea ripoti ya bodi inayoondoka afisini ya Mamlaka ya Kusimamia Utendakazi wa Polisi (IPOA), alisema uamuzi wa kupunguza walinzi hauna sababu za kisiasa.

“Gavana mmoja anahitaji walinzi 26 kwani amegeuka kuwa kituo cha polisi? Mkuu wa Polisi Joseph Boinnet na mimi si wanasiasa, jukumu letu ni kutumikia Wakenya kwa usawa,” akasema Dkt Matiang’i.

Hayo yanajiri siku chache baada ya Gavana wa Nairobi Mike Sonko kulalama kuwa walinzi wake wamepunguzwa kutoka 26 hadi watano.

Dkt Matiang’i, wiki mbili zilizopita, alisema kuwa nusu ya maafisa wa polisi wanaolinda magavana na viongozi wengineo watapunguzwa kwa asilimia 50 kufikia Julai, 2018.

“Maafisa hao watatumwa kwenda kulinda maisha na mali ya Wakenya wa kawaida katika maeneo mbalimbali ya nchi,” akasema Dkt Matiang’I kupitia mtandao wa Twitter.

Msemaji wa Polisi Charles Owino baadaye alisema kupunguzwa kwa walinzi wa Gavana Sonko ni kati ya mikakati ya kutaka kuwapokonya viongozi jumla ya walinzi 5,000 katika kipindi cha miaka miwili ijayo.

Kulingana na sheria, gavana anastahili kuwa na walinzi wasiopungua watano, hivyo wakuu wa polisi wanahisi kuwa viongozi walio na zaidi ya 20 waliwapata kwa njia isiyofaa.