Magavana wa Mlima Kenya wawatunuka sifa Spika Muturi na Jaji Mkuu Martha Koome

Magavana wa Mlima Kenya wawatunuka sifa Spika Muturi na Jaji Mkuu Martha Koome

Na CHARLES WASONGA

MAGAVANA Kiraitu Murungi (Meru), Muthoni Njuki (Tharaka Nithi) na Martin Nyaga Wambora walikutana na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi kabla ya kutawazwa kwake kama Msemaji wa Mlima Kenya kwenye hafla inayotarajiwa kesho Jumamosi.

Kwenye taarifa ya pamoja Ijumaa, magavana hao wamesema jamii ya Mlima Kenya inapaswa kupata mtu wa kuangazia masuala yanayowahusu kwa ukamilifu

“Tunahitaji mtu mkakamavu, ambaye amejaribiwa ili amsaidie Rais Kenyatta kutekeleza maendeleo yenye manufaa kwa watu wetu,” taarifa yao ikasema.

Mbw Murungi, Njuki na Wambora wameahidi kufanya kazi na Rais Kenyatta “anapoendelea kuongoza taifa hili nyakati hizi zenye changamoto nyingi.”

Wamekariri kuwa Spika Muturi amekuwa mshirika mkubwa wa Rais Kenyatta na mtu mungwana ambaye anaweza kuliongoza taifa hili na Jamii ya Mlima Kenya baada ya 2022 Kenyatta atakapostaafu.

“Tunamhimiza Muturi kufanya kila awezalo kumsaidia Rais Kenyatta aweze kufanikisha mipango ya maendeleo nchini na haswa eneo la Mlima Kenya,” taarifa yao ikasema.

Mbw Murungi, Njuki na Wambora walisema eneo la Mlima Kenya linapaswa kuwa katika meza ya kugawa rasilimali za kitaifa “ambako mustakabali wa Kenya unaamuliwa.

“Mtu ambaye anawema kutusaidia kufikia lengo hilo sio mwingine ila Justin Bedan Muturi ambaye anatoka eneo la Mlima Kenya Mashariki,” ikasema.

Magavana hao watatu walimwidhinisha Bw Muturi kuwa msemaji wa eneo la Mlima Kenya baada ya Rais Kenyatta kustaafu mnamo Agosti 2022.

Vile vile, walimpongeza Jaji Martha Karambu Koome kufuatia kuapishwa kwake kama Jaji Mkuu wa 15 wa Jamhuri ya Kenya.

Magavana hao wamemshukuru Rais Kenyatta na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) kwa kumpendekeza Koome kwa wadhifa huo.

You can share this post!

KIKOLEZO: Sema kuachwa kwa mataa

Kocha Nuno Espirito Santo kuvunja ndoa kati yake na Wolves...