Habari MsetoSiasa

Magavana wa Pwani sasa wazika tofauti zao

December 11th, 2019 2 min read

Na CHARLES LWANGA

MAGAVANA sita wa kaunti za eneo la Pwani, wameamua kuweka kando tofauti zao za kisiasa ili kukuza uchumi wa ukanda huo kupitia Jumuiya ya Kaunti za Pwani (JKP).

Mwenyekiti wa JKP, Salim Mvurya, ambaye ni gavana wa Kwale alisema serikali za kaunti zote sita yaani Kwale, Kilifi, Lamu, Taita Taveta na Tana River zinashauriana kuweka sheria na sera moja itakayovutia wawekezaji katika sekta ya Kilimo biashara na Uchumi wa Baharini.

Magavana wa kaunti hizo sita -Mvurya, Hassan Joho (Mombasa) ambaye ni naibu mwenyekiti wa JKP, Fahim Twaha (Lamu), Dhado Godhana (Tana River) Graton Samboja (Taita Taveta) na Amason Kingi wa Kilifi wanatoka vyama totauti ambavyo ni Jubilee, ODM na Wiper.

Tofauti baina ya viongozi hawa ziliyumbisha muungano wa kaunti za Pwani hasa Bw Joho ambaye ni naibu kiongozi wa ODM na Bw Mvurya ambaye alihama ODM na kuchaguliwa tena kwa tiketi ya chama cha Jubilee .

Lakini jana, kaunti zote sita zilikusanyika katika hoteli ya Ocean Beach resort, Malindi, kaunti ya Kilifi kwa kongamano la pili kuhusu uchumi wa baharini na Kilimo Biashara wakihubiri umoja, amani na ustawi.

Idadi ya waliohudhuria iliimarika kuliko kongamano la kwanza lililofanyika Julai mwaka jana.

Magavana Kingi, aliyekuwa mwenyeji wa kongamano, Bw Joho, Bw Twaha na naibu gavana wa Taita Taveta Majala Mlaghui walihudhuria ilhali Bw Godhana ambaye yuko nje ya nchi alituma maafisa wa kaunti yake kumwakilisha.

Mwaka Jumanne ni Bw Kingi, Godhana, Bw Twaha (Lamu) na Bw Majala waliohudhuria huku Mvurya na Joho wakisusia.

Tofauti zilizuka kwenye kongamano hilo kila mmoja akiwa na maoni tofauti.

Bw Kingi aliambia wajumbe kwamba lengo la kukutana lilikuwa ni kutekeleza maazimio ya mkutano wa kwanza wa JKP kuhusu Kilimo biashara na Uchumi wa baharini

“Kama kaunti binafsi, hatuwezi kuwa na ushawishi mkubwa lakini tukiungana pamoja kama ndugu na dada kuwa muungano wa kiuchumi tutaafikia mengi,” alisema.

Maridhiano

Bw Joho ambaye alihasimiana na Bw Mvurya na hata kumkumbusha kwamba alikuwa naibu mwenyekiti wa JKP, alisema kuna haja ya kushirikiana ili kuafikia lengo moja kama eneo.

“Muungano wetu wa kiuchumi utatuwezesha kutatua masuala chungu nzima yanayoathiri uwezekezaji eneo la pwani na kuvutia wawekezaji,” alisema na kuongeza “wakati bandari ya Mombasa ilijengwa, lengo lilikuwa viwanda na kuuza bidhaa nje lakini baadaye tulianza kutegemea bidhaa kutoka nje.”

Bw Mvurya alisema lengo kuu la JKP ni kuhakikisha uchumi wa pwani umestawi na kufanikisha utoaji wa huduma.Alimpongeza Rais Uhuru Kenyatta kwa kupatia uchumi wa baharini kipaumbele alipozindua kikosi cha kulinda pwani ya Kenya (KCGS).

Bw Mvurya pia aliunga ombi la Bw Kingi kwamba tatizo la maskwota eneo la pwani linapaswa kutatuliwa ili wakazi wapate vyeti vya kumiliki mashamba waweze kufanikisha uwekezaji na kupigana na umasikini.Naye Bw Twaha walikaribisha wawekezaji Lamu ambako bandari mpya inajengwa chini ya mradi wa Lapsset.