Habari MsetoSiasa

Magavana wafisadi kusimamishwa kazi wakichunguzwa

March 13th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MAGAVANA na maafisa wakuu serikalini walioshtakiwa kwa ufisadi watalazimishwa kuondoka afisini kwa muda hadi mahakama zitakapoondolea lawama.

Hii ni endapo mabadiliko ya sheria ya uhalifu inayopendekezwa na Kamati Shirikishi ya Kupambana na Ufisadi (MAT) itapitishwa na mabunge yote mawili; Seneti na bunge la kitaifa.

Jumatano, kamati hiyo inayoongozwa na Mwanasheria Mkuu Paul Kihara Kariuki iliwasilisha pendekezo hilo mbele ya kamati ya seneti kuhusu sheria na haki za kibinadamu.

MAT inataka Sheria kuhusu Maadili na Uongozi wa Maafisa wa Serikali miongoni mwa sheria husika zifanyiwe marekebisho ili kuziba mwanya ambao umekuwa ukitumiwa na mahakama kuwaruhusu maafisa walioshtakiwa au wanaochunguzwa kwa tuhuma za ufisadi kuendelea kushikilia nyadhifa zao.

“Hali hii ya maafisa wakuu kama magavana kuendelea kushikilia vyeo vyao licha ya kushtakiwa au kuchunguzwa inahujumu uchunguzi na ukusanyaji wa ushahidi dhidi yao. Watu hawa wanaweza kutumia mamlaka ya afisi zao kuwahangaisha mashahidi,” Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Nordin Haji akasema.

“Kwa hivyo, tunawaomba nyie maseneta na wenzenu wa bunge la kitaifa kuziba pengo hili la kisheria ili maafisa kama hawa walazimishwe kukaa kando kwa muda hadi uchunguzi au kesi dhidi yao zitakapokamilishwa,” akasema.

Bw Haji alitoa mfano wa Gavana wa Migori Okoth Obado ambaye licha ya kukabiliwa na mashtaka ya mauji ya aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo Sharon Otieno na anaendelea kuchunguzwa kuhusu sakata ya wizi ya Sh2.1 bilioni katika kaunti hiyo, mahakama iliamuru kwamba aachiliwe huru kwa dhamana.

“Mfano, mwingine ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) Profesa Mohammad Swazuri ambaye aliachiliwa kwa dhamana na mahakama kabla ya uchunguzi dhidi yake kuhusu sakata ya ulipaji ridhaa ya Sh234 milioni kwa ardhi ya serikali kukamilishwa,” akaongeza.

Hata hivyo, mwenyekiti wa Kamati hiyo Bw Samson Cherargei na maseneta; James Orengo (Siaya), Mithika Linturi (Meru) walionya kuwa marekebisho hayo ya kisheria yafanywe kwa uangalifu ili kutokinzani na kipengee cha Katiba kinacholinda washtakiwa.