Habari MsetoSiasa

Magavana wahepa Ruto wakihofia kuandamwa

November 13th, 2019 1 min read

Na NDUNGU GACHANE

MAGAVANA kutoka eneo la Mlima Kenya wameanza kumhepa Naibu Rais William Ruto wakiogopa kujipata katika hali sawa na wenzao walioshtakiwa kwa madai ya ufisadi.

Magavana waliozungumza na Taifa Leo kwa sharti hatutaja majina yao, walidai kumekuwa na watu wenye ushawishi katika serikali ya Jubilee wanaowatisha.

Walisema watu hao wanawatisha wakitaka wahame kambi ya Dkt Ruto au wafunguliwe mashtaka ya ufisadi.

Hii imewafanya wasusie hafla za Dkt Ruto anapotembelea kaunti zao.Miongoni mwa magavana ambao wamemuunga mkono Dkt Ruto na baadaye wakashtakiwa ni Ferdinard Waititu( Kiambu), Moses Kasaine (Samburu) na Stephen Sang (Nandi), ambao walinyamazishwa kwa kufunguliwa kesi.

Mnamo Juni, wabunge wanaomuunga Dkt Ruto chini ya vuguvugu la “Tangatanga” walilalamika kuwa kulikuwa na njama ya serikali kuwanyamazisha.

Mbunge wa Kandara, Alice Wahome aliambia Taifa Leo kwamba serikali ilikuwa imefufua kesi iliyomkabili 2012 na Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) ilikuwa tayari kumshtaki.Bi Wahome alisema masaibu ya magavana Kasaine, Sang na Waititu yalitokana na uhusiano wao na Dkt Ruto.

Gavana mmoja kutoka Mlima Kenya alieleza Taifa Leo kwamba waliamua kumhepa Dkt Ruto kwa ajili ya usalama wao wenyewe ili wasisingiziwe mashtaka ya ufisadi.

“Unajua vyema nikiwa na chuki nawe, bila shaka nitakupata. Kuna mtindo ambao wanaomuunga Dkt Ruto wanaandamwa,” gavana mmoja akasema.Gavana wa Meru, Kiraitu Murungi alisema hakutaka kuzungumzia suala hilo.