Habari MsetoSiasa

Magavana wajitetea dhidi ya shutuma za kupiga kambi Nairobi

April 11th, 2019 2 min read

Na KENNEDY KIMANTHI

MAGAVANA waliokashifiwa kwa kuendesha shughuli za kaunti zao wakiwa Nairobi, wamejitetea kwamba walilalamika kwa serikali kuu kuhusu mikutano mingi wanayoalikwa kuhudhuria jijini humo lakini hawakusikilizwa.

Kwenye barua iliyotumwa kwa Mkuu wa Utumishi wa Umma, Bw Joseph Kinyua mwaka uliopita, Baraza la Magavana lililalamika kuwa mikutano hiyo hutatiza utoaji huduma katika kaunti zao kwa sababu mingi huwa haijapangwa mapema.

Barua hiyo iliyoandikwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa baraza hilo, Bw Josphat Nanok iliomba mialiko yote ya kuhudhuria mikutano au shughuli nyingine zozote itumwe kwao angalau mwezi mmoja kabla ya mkutano wenyewe.

“Kuna mikutano mingi mno ambayo huhitaji viongozi wa kaunti na maafisa wao wahudhurie. Huwa haishangazi kupata wizara moja ikialika afisa wa kaunti kwa mikutano zaidi ya moja katika mwezi mmoja.

Hii inamaanisha maafisa wa kaunti wakati mwingi hawako afisini mwao, hali ambayo hutatiza utoaji huduma katika kaunti,” akasema Bw Nanok kwenye barua iliyoandikwa Mei 17, 2018.

Ingawa ugatuzi ulinuia kupeleka huduma na rasilimali mashinani, magavana wengi bado huendesha shughuli za kaunti zao wakiwa Nairobi.

Barua hiyo ambayo pia ilitumwa kwa mawaziri wote wa serikali kuu iliomba mwaliko wowote kwa magavana au maafisa wa kaunti utiwe sahihi na waziri anayehusika au katibu wa wizara husika.

“Baraza limeagiza maafisa wa usimamizi na serikali za kaunti kukataa mwaliko wowote ambao haufuati mwongozo huu,” barua hiyo ikasema.

Wiki iliyopita, Mwenyekiti wa baraza hilo, Bw Wycliffe Oparanya alitetea wenzake na kusema haiwezekani kusimamia kaunti bila kuzuru Nairobi mara kwa mara.

“Ukweli ni kwamba ugatuzi haujakamilika. Bado unaendelea kukua kwa hivyo tutaendelea kuja Nairobi kwani huduma nyingi tunazotegemea bado ziko huku,” akasema.

Afisa Mkuu Mtendaji wa baraza hilo, Bi Jacqueline Mogeni alisema sheria inayohusu ushirikiano kati ya serikali kuu na za kaunti inatoa mwongozo kuhusu jinsi ushirikiano huo unapaswa kufanywa.

“Kutokana na kuwa majukumu mengi ya serikali kuu na huduma hazijakabidhiwa kikamilifu kwa serikali za kaunti, imekuwa kawaida kwamba mikutano mingi na serikali kuu au hata washirika wa maendeleo hufanywa Nairobi.

Isitoshe, mikutano mingi huandaliwa na serikali kuu,” akasema.

Jana, baadhi ya magavana walihudhuria mkutano kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Kusaidia Miji ya Kenya na maandalizi ya awamu ya pili ya utekelezaji wa mpango wa kuboresha mitaa ya mabanda Nairobi.

Baadhi ya magavana walio wanachama wa kamati ya kilimo katika Baraza la Magavana pia walikutana Machi 25 huku wengine wa Kamati ya Afya wakikutana Nairobi siku nne zilizotangulia.

Imedaiwa magavana hutumia mamilioni ya pesa kila mwaka kusafiri Nairobi kwa shughuli hizo huku wengine wakiwa wamekodisha afisi jijini humo, hali ambayo inaonekana kama ufujaji wa pesa za umma.