Habari MsetoSiasa

Magavana wakaangwa kutaka wasikamatwe wakiiba mali ya umma

July 11th, 2018 2 min read

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wamelikashifu Baraza la Magavana (CoG) kwa kumtetea Gavana wa Busia Sospeter Ojaamong aliyeshtakiwa kwa ufisadi, wakilitaka baraza hilo kuunga mkono vita dhidi ya ufisadi.

Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi na masenata Mutula Kilonzo Junior (Makueni) na Mithika Linturi (Meru) pia walimsuta mwenyekiti wa baraza hilo Josephat Nanok kwa kupendekeza kuwa magavana wanapasa kukingwa dhidi ya mashtaka sawa na Rais.

“Baraza la Magavana ni asasi ambayo ilibuniwa na katiba kwa ajili kulinga na kutetea ugatuzi sio kulinda washukiwa wa ufisadi. Magavana hawafai kutumia asasi inayofadhiliwa kwa pesa za umma,” Bw Wandayi akawaambia wanahabari Jumanne katika majengo ya bunge.

“Hakuna uwajibikaji wa pamoja katika suala la ufisadi. Kila mtu afaa kuubeba msalaba wake. Na mahakama pamoja na asasi za kupambana na ufisadi zinafaa kupewa nafasi kufanya kazi zao bila kuingiliwa,” akasema Mbunge huyo ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu (PAC).

Naye seneta Linturi aliwaambia magavana kwa hawawezi kupewa kinga dhidi ya mashtaka chini ya Katiba ya sasa, akisema hadhi hiyo imepewa Rais pekee.

“Bw Nanok na wenzake waliozungumza jana (Jumatatu) hawafai kutetea pendekezo la kwa kutumia mfano wa Nigeria, ambayo ni miongoni mwa nchi fisadi zaidi duniani. Wajue katika mataifa yenye serikali za ugatuzi kama vile Amerika, Canada na Afrika Kusini, magavana hawana kinga dhidi ya mashtaka,” akasema seneta huyo ambaye ni mwanachama wa Kamati ya Seneti kuhusu Uhasibu na Uwekezaji (CPAIC).

Bw Linturi na Kilonzo Jr walisema kuwa pendekeza la Bw Nanok na wenzake linaweza tu kutekelezwa kupitia mabadiliko ya katiba hatua ambayo waliapa tulipinga.

“Nitalipinga mswada kama huo endapo utawasilishwa katika seneti. Naamini wenzetu katika bunge la kitaifa pia watakataa wazo kama hilo,” akasema Bw Kilonzo Jr.

Mnamo Jumatatu Bw Nanok ambaye pia ni Gavana wa Turkana alipendekeza kuwa magavana walindwe kisheria kutokana na mashtaka yoyote wakiwa afisini, anavyotendewa Rais wa taifa.

Akiwa ameandamana wenzake; Paul Chepkwony (Kericho), Wycliffe Oparanya (Kakamega) na Ojaamong’ Bw Nanok alilalamikia jinsia gavana huyo alivyokamatwa wiki jana, akisema alidhalilishwa.

Bw Ojaamong’ alikamatwa wiki jana na maafisa wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) alipojiwasilisha katika afisi zake Nairobi.

Alifikishwa mahakamani Ijumaa na kuachiliwa huru kwa dhamana baada ya kusomewa kosa la kupeana zabuni ya uzoaji taka ya thamani ya Sh8 milioni kinyume cha sheria.

“Mwenzetu hapa alikamatwa kwa njia ya kudunisha zaidi mbele ya kamera za wanahabari hata baada ya kujiwasilisha katika makao makuu ya EACC. Hiyo inaashiria kuwa vita dhidi ya ufisadi imeingizwa siasa,” Bw Nanok akawaambia wanahabari katika makao makuu ya CoG, Nairobi.

Alisema serikali za kaunti huwa ziko huru na utendakazi wao hazifai kuingiliwa kwa njia ambayo inaweza kutatiza shughuli zao.

“Mwelekeo bora ni katika mataifa yaliyokumbatia ugatuzi ni kwamba wakuu wa serikali kuu na zile za kaunti hupewa kinga ya mashtaka ya makosa ya kijamii na kihalifu wanapokuwa afisini,” akasema Bw Nanok.

Lakini Bw Wandayi jana alimwambia Nanok na wenzake kwamba kama mameneja wa kaunti zao wanafaa kuwajibikia matumizi mabaya ya fedha.

“Hili pendekezo la kutaka kinga ni kisingizio cha kutaka kuendelea kupora pesa za umma huku wananchi wakiendelea kuteseka kwa kukosa huduma,” akasema.

Mbunge huyo wa ODM aliwataka magavana hao kutoa nafasi kwa mahakama kufanya kazi yake hadi mwisho akiwataka kukoma kutoa matamshi yanayofasiriwa katika vitisho kwa asasi hiyo.