Habari MsetoSiasa

Magavana wakejeli ripoti kuwahusu, watisha kushtaki waliofanya utafiti

September 18th, 2019 2 min read

Na CAROLYNE AGOSA

BARAZA la Magavana (CoG) limepuuzilia mbali ripoti ya shirika moja la Uingereza kuhusu utendakazi wa magavana, likisema kuwa ni feki.

Katika taarifa Jumatano, baraza hilo lilisitiza kwamba ripoti ya shirika la All Africa Advisors (AAA) inanuia kuwachafulia jina magavana pasipo msingi wowote.

“Baraza la Magavana (CoG) limepuuzilia mbali ripoti iliyotolewa na shirika linalodai kuwa la mjini London, All Africa Advisors (AAA) kuhusu utendakazi wa Serikali za Kaunti za Kenya.

“Hii ni njama ya kisiasa kutia doa uongozi wa kaunti. Serikali za kaunti haziwezi kulinganishwa kwani kila moja ni ya kipekee na kila moja ikon a changamoto na mafanikio yake,” alisema Mwenyekiti wa CoG Wycliffe Oparanya.

Ripoti hiyo kwa jina “Effectiveness of Devolution in Kenya: 2013-2019” ilimuorodhesha Gavana wa Machakos Alfred Mutua kama bora zaidi nchini kwa alama 460.

Alifuatiwa na Bw Oparanya, ambaye ni Gavana wa Kakamega, kwa alama 440 huku Gavana wa Nairobi Mike Sonko akichukua nafasi ya tatu kwa alama 406.

Nafasi ya nne ilimuendea Gavana Kivutha Kibwana wa Makueni aliyezoa alama 374 baye Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho akafunga ukurasa wa tano bora kwa alama 345.

Shirika la AAA lenye makazi yake jijini London, Uingereza, hujishughulisha na miradi ya kibiashara na maendeleo barani Afrika.

Mkuu wa Utafiti Bw Steven Kanyatte alisema kuwa walitumia mbinu tatu katika utafiti wao.

“Kwanza kulikuwa na uchambuzi wa kila kaunti, hatua ya pili ikawa kura ya maoni katika kila kaunti kabla kukamilisha kwa zoezi la kuthibitisha miradi ya maendeleo ya kila kaunti,” alieleza Bw Kanyatte Jumanne katika hafla ya kuzindua ripoti hiyo mjini Nairobi.

Utafiti huo, uliofanywa kuanzia Juni hadi Agosti mwaka huu katika kaunti zote 47, ulinakili changamoto ambazo kila kaunti inakumbana nazo.

Bw Kanyatte aeleza kuwa vigezo vilivyotumika ni pamoja na uongozi bora, miundo msingi, upatikanaji wa maji safi, huduma za afya, makazi na nyumba, chakula cha kutosha, uwekezaji, utengenezaji bidhaa, huduma za kijamii na huduma za dharura.

Vile vile, vipimo vya ukuaji wa miji, miradi ya kukomesha umaskini, hamasisho na nafasi za uwekezaji kwa vijana na wanawake viliangaziwa.

“Watu 10 walihojiwa katika kila mji au kijiji, hususan siku za soko. Jumla ya watu 1,410 walihojiwa. Maelezo na mianya iliyopatikana itachangia kusaka miradi mbadala kwa miaka minne ijayo. Tunatumai ripoti itachangia ufahamu wa matokeo ya ugatuzi nchini Kenya,” akasema mkuu huyo.

Hata hivyo, Bw Oparanya alitilia shaka mbinu iliyotumiwa katika utafiti huo akisema hakuna serikali yoyote ya kaunti ilipokea maswali ya mahojiano yanayodaiwa kutolewa.

“Kigezo kimoja hakiwezi kutumiwa kutathmini utendakazi wa serikali zote 47 za kaunti. Inasikitikisha sana na sio sawa; na inaibuka kuwa kisa cha kuhukumiwa pasipo kujitetea,” akasema gavana huyo wa Kakamega.

Aliongeza: “Tunataka msahama mara moja kutoka kwa Bw Steven Kanyatte na kampuni yake, na wakikosa kufanya hivyo Baraza litawashtaki. Tunahimiza vyombo vya habari kutoangazia mashirika haya feki ya kura za maoni.”

Kwenye utafiti huo Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu ndiye aliyeshika mkia kwa alama hasi 615 (-615).

Cyprian Awiti (Homa Bay), Sospeter Ojaamong (Busia), Fahim Twaha (Lamu), Amason Kingi (Kilifi) na John Nyagarama (Nyamira) walifunga orodha ya magavana sita waliofanya vibaya zaidi.

Bw Awiti alizoa alama 180, Bw Ojaamong alama 136, Bw Twaha pointi 91, Bw Kingi pointi 91 na Bw Nyagarama alama 85.

Shirika la AAA linanuia kufanya utafiti mwingine 2023 kutathmini hatua ambazo serikali za kaunti zitakuwa zimefanya kuhusu maendeleo mashinani katika miaka minne ijayo.