Habari Mseto

Magavana walalamikia kucheleweshwa kwa hela

November 21st, 2020 1 min read

Na SHABAN MAKOKHA

MAGAVANA sasa wanadai kucheleweshwa kwa fedha za kaunti kumechangia pakubwa ongezeko la maambukizi ya Covid-19 mashinani.

Magavana wanadai hawana pesa za kuwanunulia vifaa vya kujikinga (PPE) maafisa wanaotoa huduma za afya.

Madaktari wanasema ukosefu wa vifaa bora vya kujikinga umewafanya waambukizwe corona.

Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Wycliffe Oparanya alisema kaunti zimekosa fedha kwa vile hazijapata mgao kutoka serikali ya kitaifa tangu Agosti 2020.

Bw Oparanya alisema kaunti zinakabiliwa na changamoto chungu nzima kutokana na ukosefu wa fedha ilhali wananchi wanataka kupata huduma.

Bw Oparanya aliitaka bunge la seneti limwagize Waziri wa Hazina Ukur Yatani afike mbele yake kueleza kinachosababisha kucheleweshwa kwa fedha za kaunti.

Alikuwa akihutubu Mumias wakati wa maombi ya mazishi ya aliyekuwa afisa wa kaunti ya Kakamega Bw Robert Sumbi.