LEONARD ONYANGO: Magavana waliofuja fedha za corona waandamwe

LEONARD ONYANGO: Magavana waliofuja fedha za corona waandamwe

Na LEONARD ONYANGO

KILA mara magavana wanapohutubia Wakenya kuhusiana na hali ya ugonjwa wa corona katika kaunti zao, wanaangua kilio badala ya kutoa suluhisho.

Huku Wakenya wakingojea kusikia idadi ya vitanda vilivyoongezwa na magavana katika vyumba vya wagonjwa mahututi (ICU), kwenye hospitali wanazozisimamia, wakuu hao wa kaunti hujitokeza kulalamikia uhaba wa vitanda.

Je, wanataka wananchi wafanye mchango wa kununua vitanda vya ICU?Wiki iliyopita, wakuu hao wa kaunti, kupitia kwa mwenyekiti wa Kamati ya Afya ya Baraza la Magavana Anyang’ Nyong’o, walilalamikia ukosefu wa vifaa vya kupima virusi vya corona katika kaunti zao.

Magavana wiki mbili zilizopita, walisema kuwa vimesalia vitanda 259 pekee vya ICU katika kaunti 42 zilizo nje ya kaunti tano zilizo kwenye eneo lililo na visa vingi vya maambukizi ya corona.

Kaunti tano zilizofungwa ili kuzuia maambukizi ya corona ni Nairobi, Kajiado, Kiambu, Nakuru na Machakos. Wakati wa kupiga marufuku kuingia au kutoka katika kaunti hizo tano, Rais Uhuru Kenyatta alisema kuwa zimesalia na vitanda 58 pekee katika vyumba vya ICU.

Hiyo inamaanisha kuwa humu nchini kuna vitanda vya ICU visivyozidi 300 ambavyo viko wazi.Inaonekana serikali yetu na magavana hawajajifunza lolote kutoka kwa mataifa kama vile India, Brazil au Iran ambayo yamelemewa na idadi kubwa ya wagonjwa wa corona.

Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali iliyotolewa hivi karibuni, inaonyesha kuwa zaidi ya Sh7.7 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya kupambana na janga la corona zilifujwa.

Kulingana na ripoti, wakuu hao wa kaunti walitoa kandarasi ya vifaa vya kukabiliana na corona kwa watu ambao hawajahitimu na waliagiza vifaa kutoka kwa kampuni za kibinafsi badala ya Mamlaka ya Kusambaza Dawa na Vifaatiba (Kemsa), kati ya maovu mengineyo.Katika hotuba zao za mara kwa mara, magavana wamesalia kimya kuhusiana na ripoti hiyo ya mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali Nancy Gathungu.

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EAC) na Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) zinafaa kuingilia kati na kuwakamata magavana waliofuja fedha za umma zilizotengewa vita dhidi ya corona.

Fedha hizo zilifaa kutumiwa kununua vifaa ambavyo vingetumika katika hospitali zinazotumiwa na wananchi wasiomudu gharama ya matibabu katika hospitali za kibinafsi.

You can share this post!

Korti yamzima Orengo kuwa wakili wa Manduku

Raila amwomboleza mwanahabari shupavu Philip Ochieng’