Habari

Magavana wamtetea vikali Koffi Olomide kutumbuiza nchini

April 17th, 2018 2 min read

Na BENSON AMADALA

GAVANA wa Kakamega, Bw Wycliffe Oparanya, amemwomba Waziri wa Ugatuzi, Bw Eugene Wamalwa, aingilie kati ili mwanamuziki mashuhuri Koffi Olomide aruhusiwe kutumbuiza wageni watakaohudhuria warsha ya ugatuzi.

Bw Olomide, ambaye jina lake halisi ni Antoine Christophe Agbepa Mumba, alifurushwa nchini Julai 2016, baada ya kuonekana kwenye video akimpiga teke msichana aliye kwenye bendi yake katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta, Nairobi.

Bw Oparanya alimwomba waziri ashauriane na mwenzake wa usalama, Dkt Fred Matiang’i, ili mwanamuziki huyo apewe kibali cha kuingia nchini.

“Watu wetu wanapenda muziki wa Koffi Olomide na itakuwa furaha sana kama mwanamuziki huyo ataruhusiwa kuja kutumbuiza katika uwanja wa Bukhungu,” akasema gavana huyo.

Bw Wamalwa ambaye alikuwa anaarifiwa kuhusu maandalizi ya warsha hiyo yalipofika aliahidi kufuatilia suala hilo na kuhakikisha Bw Olomide na wenzake wataruhusiwa kuingia Kenya.

Jumanne, Msemaji wa Wizara ya Usalama wa Ndani, Bw Mwenda Njoka, alisema waandalizi wa ziara ya mwanamuziki huyo wanahitajika kuwasilisha ombi kutaka marufuku aliyowekewa iondolewe ndipo utathmini ufanywe kuona kama ataruhusiwa kuja nchini.

“Wakati mtu anapofurushwa huwa ni jukumu la aliyefurushwa kuomba marufuku dhidi yake itolewe na aeleze sababu zake. Jukumu ni la Koffi Olomide kuwasilisha ombi na wala si la serikali,” akasema Bw Njoka.

Kulingana naye, mwanamuziki huyo alifurushwa nchini kwa njia rasmi za kisheria na hivyo basi marufuku inayomzuia kuingia nchini haiwezi kuondolewa kupitia kwa ombi la matamshi kwa waziri wa usalama.

Mkuu wa mawasiliano katika Kaunti ya Kakamega, Bw Dickson Rayori, alisema ziara ya mwanamuziki huyo haifadhiliwi na serikali ya kaunti bali waandalizi wa tamasha za burudani.

“Serikali ya kaunti haitatumia senti zozote kumleta Koffi Kakamega. Kwanza kaunti itanufaika kwa mapato kutokana na ada za kiingilio na ukodishaji wa uwanja wa michezo kwa tamasha hiyo ya Koffi,” akasema Bw Rayori.

Alipuuzilia mbali uvumi kwamba serikali ya kaunti ilitenga Sh20 milioni kumleta mwanamuziki huyo nchini.