Magavana wanuia kunyonya raia baada ya 2022

Magavana wanuia kunyonya raia baada ya 2022

Na SILAS APOLLO

MAGAVANA ambao wamehudumu kwa vipindi viwili, kila mmoja, watapokea Sh11.1 milioni kama malipo ya kustaafu, ikiwa wabunge watapitisha mswada uliopendekezwa na madiwani.

Magavana hao pia watakuwa wakipokea pensheni ya Sh739,200 kila mwezi ikiwa mswada huo utapitishwa.

Mswada huo umependekezwa na Baraza la Maspika wa Kaunti (CAF), ambalo huwajumuisha maspika wa kaunti zote 47 nchini.

Lengo lake ni kuhakikisha magavana, manaibu wao, maspika wa mabunge ya kaunti na madiwani wanapata donge nono watakapoondoka mamlakani.

Mapendekezo hayo yatajumuishwa kwenye Mfumo wa Malipo ya Uzeeni ya Maafisa wa Serikali za Kaunti.

Kwenye mapendekezo hayo, gavana aliyehudumu kwa mihula miwili atapokea kitita kitakachohesabiwa kama kiwango cha mshahara wake kwa mwaka mmoja.

Hata hivyo, kiwango hicho ni cha juu ikilinganishwa na kile kilichopendekezwa na mashirika ya serikali kama vile Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC).

Magavana pia watakuwa wakipokea malipo maalum kila mwezi, yanayolingana na asilimia 80 ya mshahara wao wa mwisho walipokuwa uongozini.

Watalipwa fedha hizo maisha yao yote baada ya kuondoka afisini.Ikiwa gavana atafariki baada ya kuondoka uongozini, mswada huo unapendekeza malipo hayo kupewa mkewe au wanawe katika maisha yao yote.

Naibu gavana aliyestaafu atalipwa kitita kinacholingana na jumla ya mshahara wake kwa mwaka mmoja. Vilevile, atakuwa akipokea malipo ya kila mwezi yanayolingana na asilimia 60 ya mshahara aliokuwa akipokea.

Kiwango hicho ni sawa na fedha ambazo maspika wa mabunge ya kaunti watakuwa wakipokea. Kulingana na takwimu za sasa, gavana huwa anapokea Sh924,000 kama mshahara kila mwezi.

Hilo linamaanisha atapokea Sh11.1 milioni, kwani ndizo zinazolingana na jumla ya mshahara wao kwa mwaka mmoja.

Manaibu wao watapokea Sh7.4 milioni kila mmoja na Sh373, 750 kila mwezi. Maspika watapokea Sh3.1 milioni na Sh155, 925 kama pensheni kila mwezi.

Kwa sasa, maspika hao hulipwa mshahara wa Sh259, 857 kila mwezi. Madiwani nao watapokea Sh1.7 milioni. Kwa sasa, madiwani huwa wanalipwa Sh144, 375 kila mwezi.

You can share this post!

Korti sasa kuamua hatima ya kesi kuhusu CBC

Ruto ataka wabunge wasipoteze muda wakifufua BBI