Habari MsetoSiasa

Magavana waomba wasikamatwe kwa ufisadi

July 10th, 2018 1 min read

Na VALENTINE OBARA

MAGAVANA wanataka wasiwe wakikamatwa wanapohusishwa na kashfa za ufisadi kwa sababu mamlaka yao yanastahili heshima.

Kupitia kwa Baraza la Magavana, wakuu hao wa kaunti jana walilalamikia jinsi Gavana wa Busia, Bw Sospeter Ojaamong, alivyokamatwa wiki iliyopita wakisema aliaibishwa.

Mwenyekiti wa baraza hilo Josphat Nanok alisema sawa na jinsi rais anavyolindwa kisheria kutokana na mashtaka yoyote anapokuwa mamlakani, inapaswa magavana pia walindwe kwani wao ni wakuu wa serikali za kaunti.

Kwenye taarifa aliyosoma kwa niaba ya wenzake, gavana huyo wa Kaunti ya Turkana alisema serikali za kaunti huwa ziko huru na utawala wao haupaswi kuingiliwa kwa njia inayotatiza shughuli za ugatuzi.

“Mwelekeo bora katika mataifa yaliyo na ugatuzi ni kwamba wakuu wa serikali kuu na za kaunti wanafaa kuwa na ulinzi dhidi ya mashtaka ya kijamii na kihalifu wakati wanapokuwa mamlakani,” akasema.

Alikuwa akizungumza kwenye kikao cha wanahabari katika afisi za baraza hilo jijini Nairobi.

Bw Ojaamong alikamatwa na maafisa wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) Jumatano iliyopita kwa madai ya ufisadi katika utoaji zabuni ya uzoaji taka.

Alikamatwa alipojisalimisha katika makao makuu ya EACC, akafungiwa seli kisha baada ya saa nne akafungwa pingu na kupelekwa katika Mahakama ya Milimani. Aliachiliwa kwa dhamana.

Pamoja na washtakiwa wengine watatu ambao ni maafisa wa kaunti yake, waliachiliwa Ijumaa kwa dhamana ya Sh1 milioni pesa taslimu kila mmoja.

Bw Nanok alisema ingawa magavana wanaunga mkono vita dhidi ya ufisadi, inafaa waheshimiwe sawa na jinsi maafisa wa serikali kuu wanavyofanyiwa wakati wanapohusishwa na madai ya ufisadi.

“Wakati mawaziri wanapohusishwa na ufisadi, huwa wanasimamishwa kazi kimyakimya. Heshima hii hutupwa nje wakati gavana anapojikuta katika hali kama hii,” akasema.