Magavana watafutia wachumba wao mlo

Magavana watafutia wachumba wao mlo

BENSON AMADALA Na BENSON MATHEKA

MAGAVANA wameanza mikakati ya kutafutia waume na wake zao minofu katika serikali za kaunti kwa kuwateua kushikilia nyadhifa tofauti na kuanzisha afisi zinazofadhiliwa na pesa za mlipa ushuru.

Katika hatua inayoweza kufungulia wachumba wengine wa wakuu wa kaunti mlango wa kunufaika moja kwa moja na pesa kutoka serikali zao, Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa anataka Bunge la Kaunti hiyo kupitisha sheria ya kubuni Afisi ya Mke wa Gavana.

Akihutubia madiwani wa bunge hilo Jumanne, Bw Barasa alisema serikali yake inatambua wajibu wa mkewe katika kumsaidia kutekeleza majukumu yake na anaweza kufanya hivyo kupitia ofisi iliyoanzishwa kisheria.

Bw Barasa alisema anafahamu hakuna sheria inayompatia idhini ya kubuni ofisi hiyo na akaomba madiwani kuipitisha tena kwa haraka.

Mkewe Profesa Janet Kassily Barasa ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Masinde Muliro na alipokuwa akishukuru wapigakura kwa kumchagua mumewe, alisema anapenda sana kushughulikia masuala yanayoathiri wanawake kando na kazi yake ya kufunza Chuo Kikuu.

Chama cha wake wa Magavana kinawaleta pamoja wake wa wakuu wa kaunti na kupitia chama hicho, wamekuwa wakihusika na utetezi wa maslahi ya wanawake na watoto, ushirikiano na shughuli za kijamii.

Kwa wakati huu, kuna wanawake saba magavana na kupitishwa kwa sheria anayoomba Gavana Barasa, kunaweza kuwachochea kuanzisha afisi na kutengewa majukumu maalumu.

Gavana wa Meru Kawira Mwangaza amemteua mkewe kusimamia Idara ya Huduma ya Vijana katika kaunti hiyo.

Ingawa Bi Mwangaza alisema mumewe hatakuwa akipokea mshahara au marupurupu yoyote kwa kutekeleza majukumu hayo, uteuzi huo uliibua hisia kali kutoka kwa wakazi na Wakenya kwa jumula.

Sawa na Bw Barasa, Bi Mwangaza alitetea hatua yake akisema mumewe alichangia katika ushindi wake na anapenda sana maslahi ya vijana.

Bw Barasa alisema , mkewe atamsaidia kutimiza ajenda zake katika miaka mitano ijayo alizotaja kama afya, utoshelevu wa chakula, kuunda utajiri, elimu ya chekechea, ustawi wa jamii na utawala bora.

Ibara ya 185(2) ya Katiba ya Kenya 2010 inapatia Bunge la Kaunti mamlaka ya kuunda na kupitisha sheria za kuwezesha magavana kutekeleza majukumu ya serikali za kaunti.

“Aidha, ibara ya 235 (1) (a) ya katiba inatoa mfumo wa kuanzishwa na kufungwa kwa ofisi za serikali za kaunti. Kwa hivyo, ninaomba bunge hili la heshima kuwazia na kuharakisha sheria itakayoanzisha ofisi ya mke wa gavana,” Bw Barasa alisema.

Hata hivyo, wadadisi wa siasa na utawala wanasema kwamba, ingawa sio makosa kwa magavana kusaidiwa na wachumba wao kutekeleza majukumu yao, ni wazi kuwa wanataka kuwatafutia njia za kufaidika na pesa za kaunti.

“Yamkini magavana wanataka kutumia mabunge ya kaunti kuhalalisha mikakati na mipango yao ya kuwezesha wachumba wao kunufaika na pesa za kaunti,” asema mchanganuzi wa siasa na utawala Dkt Isaac Gichuki.

Anasema kwamba, tangu 2013, wachumba wa magavana wamekuwa wakitekeleza kazi za kijamii wakiungwa na wakuu wa kaunti.

“Wanachotaka kufanya sasa ni kuhalalisha shughuli ambazo wachumba wa wakuu wa kaunti wamekuwa wakitekeleza,” asema.

  • Tags

You can share this post!

Njama ya Kenya Kwanza kuzika ODM Pwani

Wakazi walalama kuhusu ongezeko la noti feki za elfu

T L