Magavana wataka watengewe fedha za kufadhili afya, kilimo na maji

Magavana wataka watengewe fedha za kufadhili afya, kilimo na maji

Na CHARLES WASONGA

MAGAVANA wameitaka Serikali ya Kitaifa kuzitengea serikali za kaunti mabilioni ya fedha ambazo huelekezwa kwa sekta za Kilimo, Afya na Maji kama ishara ya kuonyesha kujitolea kwake kufanikisha ahadi za mswada wa BBI.

Wakiongozwa na Mwenyekiti mpya wa Baraza la Magavana (CoG) Martin Wambora, wakuu hao wa kaunti waliwataka maseneta kuisukuma Wizara ya Afya ili fedha za sekta hiyo zitengewe serikali za kaunti katika bajeti itakayosomwa Juni 2021.

“Haina haja kwa Wizara za Afya, Maji na Kilimo za Serikali Kuu kutengewa mabilioni ya fedha ilhali haya ni majukumu ambayo yamegatuliwa kwa mujibu wa Katiba. Sasa tunaitaka serikali kuu kuelekeza fedha hizi kwa serikali za kaunti katika bajeti ijayo kama ishara ya kuonyesha kujitolea kwake kutimiza ahadi ya BBI kwamba Kaunti zitengewe asilimia 35 ya mapato kila mwaka,” akasema Bw Wambora.

Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga alitoa mfano wa Sh141 bilioni zilizotengewa Wizara ya Afya katika bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2020/2021 akisema fedha ni nyingi kupitia kiasi.

“Kuna haja gani kwa Wizara ya Afya ambayo wajibu wake ni kutunga za sera pekee kutengewa Sh141 bilioni katika bajeti ya mwaka huu, ilhali majukumu megine ya sekta ya afya yanatekeleza na serikali za kaunti,” akasema Bw Kahiga.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Afya kuhusu Afya Peter Anyang Nyong’o aliwataka maseneta kuhakikisha kuwa fedha za majukumu ya afya yaliyogatuliwa yanatolewa kutoka serikali kuu na kupelekwa katika serikali za kaunti.

“Nawaomba enyi maseneta kuingilia kati na kuhakikisha kuwa Hazina ya Kitaifa inaachilia fedha zote za sekta ya afya kwani zinahitajika katika ngazi za mashinani. Fedha ziandamane na majukumu,” akasema Profesa Nyong’o.

Magavana hao walisema hayo Jumanne walipofika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Ugatuzi kujadilia kuhusu njia ya kufanikisha majukumu ya asasi hizo mbili kwa ajili ya kufanikisha ugatuzi.

Kamat hiyo inayoongozwa na Seneta wa Homa Bay Moses Kajwang’ pia ilikuwa imewaita Bw Wambora na wenzake ili wajadiliane kuhusu suala zima la utayarishaji wa Bajeti ya Kitaifa ya mwaka huu.

Magavana wengine waliohudhuria kikao hicho katika majengo ya bunge ni pamoja na Profesa Paul Chepkwony (Kericho), Dkt Wilbur Otichillo (Vihiga), Nderitu Muriithi (Laikipia), James Ongwae (Kisii) na Kiraitu Murungi (Meru).

Wakati huo huo, Wambora na wenzake waliwataka maseneta kumwagiza Waziri wa Fedha Ukur Yatani kufika mbele ya Kamati hiyo ya Seneti kuhusu Ugatuzi kuelezea kutoa maelezo kuhusu kero la kucheleweshwa kwa usambazaji wa mgao wa fedha kwa kaunti.

“Hii ni shida kubwa ambayo tungewaomba ninyi kama maseneta mtusaidie kwa kumwita Waziri wa Fedha mbele yenu. Baadhi ya kaunti huchelewe kulipa mishahara ya wafanyakazi kutokana na kucheleweshwa kwa utoaji wa fedha hizo kwa wakati,” akasema Bw Wambora.

Seneta Kajwang, aliwaahidi magavana hao kuwa Kamati yake itamwita Waziri Yatani “hivi karibuni” afike mbele yake kujadili njia za kutoa suluhu la kudumu kwa tatizo hilo.

You can share this post!

Twitter kuwazima milele wanaopotosha kuhusu chanjo ya corona

Mwanasiasa yeyote asijiapishe tena kama Raila, ni haramu...