Magavana waunda vyama vipya kuepuka baridi 2022

Magavana waunda vyama vipya kuepuka baridi 2022

Na LEONARD ONYANGO

MAGAVANA wanaohudumu muhula wa pili wamekimbilia kuunda vyama katika juhudi za kukwepa baridi ya kisiasa watakapostaafu mwaka ujao.

Kiongozi wa Kaunti ya Mandera Ali Roba ndiye gavana wa hivi karibuni kumiliki chama cha kisiasa.Gavana Roba ambaye amedokeza kuwa huenda akawania useneta wa Mandera katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022, sasa anadhibiti chama cha United Democratic Movement (UDM).

Naibu wa Rais William Ruto alipogura ODM baada ya kutofautiana na kiongozi wa chama hicho Bw Raila Odinga kabla ya uchaguzi wa 2013, alihamia UDM.

Lakini Dkt Ruto alipigwa teke baadaye na wamiliki wa UDM na kulazimika kuunda chama chake cha United Republican Party (URP) kilichovunjwa 2016 kuunda chama cha Jubilee.

Ijumaa, UDM ilitangaza kuwatimua maafisa wake wa zamani katika hatua ambayo imefasiriwa kwamba ni hatua ya Gavana Roba kudhibiti kikamilifu chama hicho.

Kulingana na orodha iliyochapishwa katika Gazeti Rasmi la Serikali la Ijumaa, mwenyekiti mpya wa UDM atakuwa Bashir Maalim Madey. Wadhifa huo ulishikiliwa na Mohamed Galgalo.

Katibu Mkuu wa UDM sasa atakuwa mwanahabari David Ohito huku Bw Paul Sigei aliyeshikilia wadhifa huo akiondoka afisini.

Mwekahazina atakuwa Abdirizak Hussen Sheik.Msajili wa Vyama vya Kisiasa Ann Nderitu amewataka Wakenya walio na pingamizi dhidi ya maafisa hao wapya wa UDM kuwasilisha kwa njia ya maandishi kufikia Ijumaa.

Gavana wa Murang’a Mwangi wa Iria tayari ameunda chama chake cha Usawa kwa Wote ambacho anatarajia kukitumia kutafuta nafasi katika serikali ijayo.

Gavana Wa Iria ametangaza kuwa atawania urais katika uchaguzi ujao kwa kutumia chama chake chenye alama ya ng’ombe wa maziwa.

Gavana Wairia anasema kuwa chama chake tayari kimefungua afisi 56 katika maeneo mbalimbali nchini.Usawa kwa Wote kwa wote ni miongoni mwa zaidi ya vyama 30 ambavyo vimekita kambi katika eneo la Mlima Kenya vikitafuta uungwaji mkono kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.

“Chama cha Usawa kwa Wote kinaendelea na shughuli ya kusajili wanachama katika eneo la Mlima Kenya na sehemu nyinginezo za nchi,” Gavana Wairia akaambia Taifa Jumapili.

Gavana wa Kilifi Amason Kingi pia anataka kutumia chama chake cha Pamoja African Alliance (PAA) kufanya mazungumzo ya muungano na ODM chake Raila Odinga.

Kulingana na mbunge wa Magarini Michael Kingi, ambaye ni kaka yake Gavana Kingi, chama cha PAA ambacho hakijapewa cheti cha kusajiliwa kamili, kitazinduliwa mwishoni mwa mwezi huu.“Chama cha PAA tayari kimefungua afisi 30 katika maeneo mbalimbali nchini,” anasema mbunge wa Magarini.

Chama cha ODM, kupitia kwa msemaji wake Philip Etale, kimetofautiana na Bw Kingi huku kikisema kuwa hakuna mazungumzo yoyote ya muungano yanayoendelea baina ya vyama hivyo viwili.

Gavana wa Migori Okoth Obado ametangaza kuwa atawania urais kupitia chama cha People Democratic Party (PDP). Juhudi za Bw Obado kutwaa chama cha PDP zimegonga mwamba baada ya kuzimwa na mbunge wa zamani wa Mugirango Kusini Omingo Magara.

Gavana wa Machakos Alfred Mutua analenga kutumia chama chake cha Maendeleo Chap Chap kuunda muungano na ODM.Kiongozi huyo wa Machakos ameimarisha ukaribu wake na Bw Odinga baada ya kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kushikilia kuwa atawania urais kivyake 2022.

Bw Odinga anapanga kujaza pengo la Bw Musyoka kwa kukumbatia magavana Dkt Mutua, Bi Charity Ngilu (Kitui) na Prof Kivutha Kibwana (Makueni) katika uchaguzi mkuu ujao.

Aliyekuwa gavana wa Kiambu William Kabogo tayari amesajili chama chake cha Tujibebe Wakenya anachonuia kukitumia kutafuta wadhifa katika serikali ijayo.

Japo Bw Kabogo ametangaza kuwa atawania urais mwaka ujao, wandani wake wanasema huenda akamenyana na Gavana James Nyoro katika kinyang’anyiro cha ugavana wa Kiambu.

Gavana Nyoro ni mwandani wa Rais Uhuru Kenyatta na Bw Kabogo aliamua kuunda chama chake kutokana na hofu kwamba huenda akanyimwa tiketi ya Jubilee.

Vingi ya vyama vinavyongojea kupewa cheti cha usajili kuwa vyama kamili vinahusishwa na magavana mbalimbali wanaohudumu muhula wa pili.

Miongoni mwa vyama 23 vinavyongojewa kupewa cheti cha kutambuliwa rasmi ni Kenya Democracy for Change, Kenya Union, Common People’s, Adopt Development Assembly, Daraja Redevelopment kati ya vinginevyo.

You can share this post!

Hizi ndizo athari za marufuku kwa wanasiasa madhabahuni

DINI: Usiogope kushindwa, hiyo ni kama giza kabla ya...