Magenge hatari tishio kwa utalii Mji wa Kale

Magenge hatari tishio kwa utalii Mji wa Kale

KWA miaka mingi, Mji wa Kale katika Kaunti ya Mombasa umekuwa mojawapo ya vivutio vikuu vya utalii kimataifa.

Hii ni kutokana na kuwepo kwa vivutio kama vile Fort Jesus, majengo na vyakula vinavyoenzi tamaduni ya Waswahili, Msikiti wa Mandhry, ambayo ndio ya zamani zaidi yaliyojengwa mwaka wa 1570, miongoni mwa mengine.

Lakini katika siku za hivi majuzi, mtaa huo umegeuka kuwa maficho ya genge la vijana wahalifu wanaotumia silaha butu kuvamia watalii wa kimataifa pamoja na wenyeji mchana peupe.

Hivi majuzi, vijana hao walinaswa kwenye kamera za CCTV, wakimvizia na mwishowe kumvamia mtalii aliyekuwa akitembea karibu na Msikiti wa Mandhry.Mwanamke huyo alijaribu kukabiliana na vijana hao waliokuwa wamebeba mabakora lakini alishindwa nguvu.

Kanda hiyo ya video ilifichua hali ambayo wakazi wa mtaa huo wanasema, imekuwa ikiendelea kwa muda sasa, na imezua wasiwasi miongoni mwa wawekezaji wa utalii, wafanyabiashara na wakazi ambao wameitaka serikali kukabiliana na vijana hao.

“Cha kusikitisha ni kuwa, hao vijana ni watoto wadogo wenye umri wa miaka kati ya 12 hadi 15. Walikuwa wanaenda shuleni hapo awali lakini walifukuzwa kwa sababu ya utovu wa nidhamu. Wametelekezwa na wazazi wao, wacha dunia iwafundishe,” alisema Bw Ahmed Abu, mkazi wa eneo hilo.

Bw Abu, mzaliwa wa Mji wa Kale, alisema kwa karibu miaka 50 ameishi Mji wa Kale, hajawahi kukumbana na utovu wa usalama kwa viwango vinavyoshuhudiwa sasa.Yeye ni mmoja wa wale ambao waliwahi kuvamiwa na magenge hayo hivi majuzi, ila alinusurika walipotambua kwamba anawajua vizuri.

“Walipogundua kuwa ninawajua na wananifahamu waliniacha nipite niende kwangu. Ilikuwa usiku nilikuwa nimetoka kazini. Nilijiuliza endapo wangelikuwa hawanijui si wangeniua? Nilishangaa namna watoto wadogo wamejiingiza kwenye uhalifu,” alisema Bw AbuBw Abu alilaumu wazazi kwa kukataa kuwapa nidhamu watoto wao, huku wengine wakisemekana kuwalinda watoto wao hata wanapofahamu ni wanachama wa magenge ya uhalifu.

Siku kadhaa baada ya kisa cha uvamizi wa watalii, maafisa wa polisi walifanya msako mkali na kuharibu maficho ya genge hilo. Hata hivyo baadhi ya vijana hao walidaiwa kukimbilia baharini na kuogolea hadi Mkomani na kujificha.

Juhudi za polisi kuwasihi wakazi na wazazi kuwapasha habari zimeambulia patupu.Afisa mkuu wa polisi Mombasa, Bw Joseph Ongaya, aliapa kukabiliana na utovu huo wa usalama akiwasihi vijana hao kujisalimisha kabla wakamatwe.

“Tumeweka juhudi zetu zote kukabiliana na utovu wa nidhamu, tunaweka maafisa wetu wa polisi Mji wa Kale kukamata wahalifu,” alisema.Mkaazi mwingine, Bw Rashid Rehan, alisema kudorora kwa usalama ni tishio la uchumi wao unaotegemea utalii.

“Tunashirikiana na wakazi wengine kuwasaka vijana hao, lakini tunasihi vyombo vya usalama kuimarisha usalama na polisi kushika doria mara kwa mara,” alisema Bw Rehan.Mwelekezi wa watalii, Bw Anthony Kahindi, alieleza wasiwasi kuwa hali ya ukosefu wa usalama itaathiri sekta ya utalii wanayoitegemea kujipatia riziki.

  • Tags

You can share this post!

Ruto apata pigo wandani wake wakiamua kujiunga na Jubilee

Kero ya ugonjwa wa misuli ya mgongo

T L