Habari

Magenge hatari yalivyoteka nchi

May 3rd, 2019 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

WAKENYA wengi wanaendelea kuishi roho mkononi huku magenge ya wahalifu yakizidi kongezeka na polisi kuonekana kushindwa kudhibiti wahuni hao.

Wahuni wanazidi kuteka uchumi wa nchi, hasa katika miji ambapo biashara kama uuzaji wa mafuta na uchukuzi wa teksi huendeshwa kwa saa 24.

Wahalifu hao wana ujasiri mkubwa hivi kwamba wanaua maafisa wa utawala, maafisa wa polisi na hata wanakijiji ambao wanachukuliwa kuwa wasaliti.

Baadhi ya magenge kama vile Gaza na 42 Brothers ambayo hapo awali yalikuwa yakihangaisha wakazi jijini Nairobi sasa yamesambaa katika maeneo mengine ya nchi, haswa maeneo ya Magharibi mwa Kenya, Kati na Pwani ambapo yameongeza hali ya wasiwasi.

Kuna madai baadhi ya magenge hayo yanafadhiliwa na wanasiasa na hivyo kuwa vigumu kwa polisi kuyakabili.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo umebaini kuwa, karibu watu 20 wameuawa na magenge ya wahalifu tangu Januari, mwaka huu.

Kisa cha hivi karibuni zaidi ni kile cha Jumanne asubuhi ambapo genge la watu wawili liliua afisa wa kampuni ya basi la Dream Line katika eneo la Magongo, Changamwe jijini Mombasa na kumwibia kiasi kisichojulikana cha fedha usiku.

Saa chache baadaye, washukiwa hao walipigwa risasi na kuuawa na polisi katika vituo vya mabasi vya Mikindani na Jomvu katika Kaunti ya Mombasa.

Polisi walipata bastola aina ya Ceska iliyokuwa na risasi sita.

Wiki iliyopita, polisi katika eneo la Rabai, Kaunti ya Kilifi, waliuawa washukiwa watatu baada ya kumvamia na kumnyang’anya mfanyabiashara Sh660,000 mchana.

Mnamo 2016, aliyekuwa waziri wa Usalama Joseph Nkaissery alitoa orodha ya magenge haramu 90 na akatangaza vita dhidi ya wahalifu hao.

Ripoti Kuhusu Hali ya Uchumi ya 2019 iliyotolewa na Shirika la Takwimu nchini (KNBS) inaonyesha kuwa, visa vya uhalifu nchini vinazidi kuongezeka kila mwaka.

Ripoti hiyo inaonyesha kulikuwa na visa 88,268 mwaka jana ikilinganishwa na 77,992 mnamo 2017.

Mwaka 2018, visa vya wizi wa mabavu vilikuwa 5,970 , uvamizi 2,935, wizi wa magari 1,370, usambazaji wa mihadarati 8,021 kati ya aina nyinginezo za uhalifu.

Uhalifu uliotokana na uuzaji wa mihadarati uliongezeka kwa asilimia 44, kutoka 5,565 katika mwaka 2017 hadi 8,021 mwaka jana.

Ripoti iliyotolewa na Kituo cha Kutafiti Uhalifu nchini mnamo 2012 ilionyesha kuwa vijana wengi wanajiunga na magenge ya uhalifu kutokana na ukosefu wa ajira, utumiaji wa dawa za kulevya kati ya sababu nyinginezo.

Jijini Nairobi, magenge kama vile Gaza, Yakuza na Smarter yamekuwa yakiwahangaisha wakazi wa maeneo ya Kayole hata majira ya mchana.

Magenge hayo hutumia visu, bunduki na silaha butu kupora maduka ya Mpesa, benki na hata kuvamia watu wanaotoka katika mashine za ATM.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo pia umebaini kuwa, kundi linalojulikana kama 40 Brothers limekuwa likihangaisha watu katikati mwa jiji la Nairobi.

Katika Kaunti za Busia na Kakamega, magenge yanayofahamika kama “Forty-Two Brothers,” na “Marach Boys” yamekuwa yakivamia na kuwajeruhi watu vijijini hata mchana.

Mnamo Machi 4, mwaka huu, kundi la Forty-Two Brothers lilihusishwa na mauaji ya mabawabu sita kwenye soko la Kilingili, Kaunti ya Busia.

Polisi katika eneo la Kati wanasema kuwa wanachama wa magenge ya Mungiki, Gaza na Usiku Sacco ambayo yamekuwa yakihangaisha wakazi wa maeneo ya Nyeri, Murang’a, Kirinyaga, Kiambu na Nyandarua ni vijana wadogo wakiwemo wanafunzi wa shule za upili.

Maafisa wa polisi wamekuwa na kibarua kigumu katika kukabiliana na zaidi ya magenge 30 ya wahalifu katika maeneo ya Pwani. Magenge hayo yanajumuisha vijana wa umri mdogo ambao wamekuwa wakivamia makazi ya watu.

Msemaji wa Polisi Charles Owino anakiri kuwa ni kibarua kigumu kuyaangamiza magenge hayo ya wahalifu huku akionya kuwa hawatakuwa na mahali pa kujificha siku za usoni.

“Ikiwa tuna uwezo wa kukabiliana na magaidi na kudumisha amani nchini, sioni kwamba genge la vijana wachache pale Kisauni au Kayole wanaweza kuwalemea polisi,” anasema Bw Owino.