HabariMakala

Magenge yateka Nyumba Kumi

February 19th, 2018 3 min read

Na MWANGI MUIRURI

Kwa Muhtasari:

  • Makundi haya yameibuka kwa visingizio kuwa yanalinda usalama, lakini badala yake yamekuwa ya wauaji
  • Kaunti za Kirinyaga, Nairobi, Kiambu, Nyamira na Murangá ndizo zinazoongoza kwenye visa hivyo vya mauaji
  • Visa hivyo vimekuwa vikizuka kwa kuwa wananchi wengi hawaelewi kuhusu lengo kamili la Nyumba Kumi
  • Wengine wanatumia makundi hayo kutatua mizozo ya kibiashara, kimapenzi, urithi na kisiasa 

MPANGO wa usalama wa Nyumba Kumi umegeuka kuwa kero baada ya kutekwa na makundi ambayo yanawaua washukiwa kiholela na kuhangaisha raia.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mpango wa Nyumba Kumi, Bw Joseph Kaguthi, makundi hayo yaliwaua watu 603 mwaka 2017.

Bw Kaguthi anaeleza kuwa makundi haya yameibuka kwa visingizio kuwa yanalinda usalama, lakini badala yake yamekuwa ya wauaji.

Makundi hayo pia yanalaumiwa kwa kuwaua watu wasio na hatia kwa kulipwa kuhangaisha baadhi ya watu kutokana na mizozo kama vile ya kifamilia, urithi na kibiashara.

Kulingana na Bw Kaguthi, kuundwa kwa kundi lolote la raia kulinda usalama ni kinyume cha sheria kwani jukumu hilo ni la polisi.

“Hakuna ruhusa kisheria kwa raia kujiunga na kundi lolote la kiusalama ama kumvamia mshukiwa na kumuua au kumpa kipigo. Washukiwa wanafaa kukabidhiwa polisi,” akasema.

Mpango wa Nyumba Kumi ulianzishwa mnamo 2013 katika juhudi za kupiga jeki ushirikiano wa raia na polisi katika kudumisha usalama.

Alieleza kuwa wajibu wa raia katika Nyumba Kumi ni kutoa habari kwa polisi na maafisa wa utawala na kuhakikisha wanawafahamu majirani zao na mienendo yao.

Akiongea na Taifa Leo katika kaunti ya Murang’a, Bw Kaguthi alisema kaunti za Kirinyaga, Nairobi, Kiambu, Nyamira na Murangá ndizo zinazoongoza kwenye visa hivyo vya mauaji ya washukiwa na watu wasio na hatia.

“Magenge hayo ya mauaji yanajiunda kwa visingizio kuwa ni ya Nyumba Kumi. Hakuna uhalali wowote wa kuua washukiwa na hakuna mahali katika mpango wetu penye mwanya wa kuundwa kwa makundi ya kijamii ya kulinda usalama,” akasema Bw Kaguthi.

 

Kaunti zilizoathirika

Kaunti ya Kirinyaga inaongoza katika mauaji ya washukiwa ikiwa na visa 62 mwaka 2017. Inafuatwa na Kisii ikiwa na visa 43, ambapo wengi wa waliouawa Kisii ni washukiwa wa uchawi.

Kimaeneo, Kati inaongoza kwa visa 187, Nyanza 126 na Nairobi 79.

Mkurugenzi wa Mpango wa Nyumba Kumi, Bw Joseph Kaguthi. Amesema makundi haramu yaliwaua watu 603 mwaka 2017. Picha/ Maktaba

Bw Kaguthi alisema kuwa ofisi yake imezindua warsha za kuhamasisha raia katika kaunti zote 47 kuhusu mbinu za kutekeleza mpango wa Nyumba Kumi bila kukiuka haki za binadamu.

Kulingana na mkurugenzi huyo, kuna baadhi ya wanasiasa na maafisa wa usalama ambao wanahusika katika magenge hayo.

Alitoa mfano wa machifu wawili na wanakamati watatu wa Nyumba Kumi katika kaunti ya Nyeri ambao walishambulia na kuua mshukiwa wa kuuza changáa katika kijiji cha Ichuga kwa madai kuwa alikaidi kukamatwa.

 

Kukwepa kushtakiwa

Alisema pia kuna mwanasiasa wa Kiambu ambaye anakinga kushtakiwa kwa jamaa wake ambaye pamoja na watu wengine waliodai kuwa wanachama wa Nyumba Kumi eneo la Ruiru walimuua Francis Kimani, 33, mwezi Novemba 2017.

Mkurugenzi wa Mpango wa Ushirika Kati ya Polisi na Raia katika kupambana na uhalifu, Philip Tuimur anasema visa hivyo vimekuwa vikizuka kwa kuwa wananchi wengi hawaelewi kuhusu lengo kamili la Nyumba Kumi.

“Nyumba Kumi haimaanishi raia wajigeuze kuwa polisi na hakimu. Wanafaa watupatie habari muhimu kuhusu uhalifu nao polisi wachunguze na kuandaa mashtaka.

Inasikitisha kuwa raia wengi wameamua kuwa kuwaua wahalifu ndio suluhu. Lakini tumekataa hilo na tutakuwa tukiwaandama wote ambao watashiriki visa hivyo kama wahalifu,” asema.

 

Mauaji kutatua mizozo

Bw Kaimur anaeleza kuwa kuna baadhi ya watu ambao wanachukua fursa ya mpango huo kuwaua watu waliokosana.

“Tunajua kuna wengine ambao wanatumia makundi hayo kutatua mizozo ya kibiashara, kimapenzi, urithi na kisiasa kwa kufadhili magenge hayo yawaue maadui kwa visingizio kuwa ni wahalifu,” akasema.

Kwa mujibu wa afisa wa shirika la Independent Medical Legal Unit (IMLU), ambalo hutetea waathiriwa wa ukiukaji wa haki za kibinadamu, Samuel Mohochi, visa vya raia kuwaua washukiwa vimetokana na wananchi kukosa imani kwenye kikosi cha polisi.

Anasema kuwa raia wengi wamepoteza imani na polisi kwa kuwa licha ya habari muhimu kutolewa kwao kuhusu uhalifu hawachukui hatua.