Habari

Magereza yamulikwa kwa kununua majaketi duni ya kuwakinga askari dhidi ya risasi

July 24th, 2019 2 min read

Na PETER MBURU

IDARA ya Magereza inamulikwa baada ya kubainika kuwa ilitumia Sh43 milioni kununua majaketi ya kuzuia risasi kwa askari wake, japo mavazi hayo hayana ubora wa kulinda askari hao wasiuawe na risasi.

Idara hiyo aidha inamulikwa kutokana na madeni ya zaidi ya Sh6 bilioni, ambazo zinasemekana kutokana na manunuzi ya vyakula na bidhaa zingine za kutumika jela, ambazo inashukiwa hazikuwahi kununuliwa.

Maswali hayo yaliibuka Jumanne wakati maafisa wa idara hiyo walifika mbele ya Kamati ya Bunge Kuhusu Uhasibu (PAC), kueleza kuhusu matumizi ya pesa.

Katibu Zeinab Hussein alikiri kuwa idara hiyo ilinunua majaketi hayo kwa gharama ya Sh22 milioni, pamoja na vesti za kujikinga kutokana na risasi kwa Sh21 milioni.

Hata hivyo, aliendelea kusema kuwa mavazi hayo hayakuwa na ubora unaohitajika ili kumkinga mtumizi kutokana na risasi ama silaha zingine kama kisu.

Ukaguzi wa mavazi hayo katika maabara ulibaini kuwa yana uwezo wa kumkinga mtumizi kutokana na risasi za bunduki zenye uwezo wa kufyatua umbali wa karibu tu.

Lakini katibu huyo alitetea kuwa mavazi yenyewe yalinunuliwa kwa mafunzo katika chuo cha uaskari, wala si ya kutumiwa kazini na skari.

“Manunuzi yaliyofanywa yalikuwa ya majaketi ya kukinga risasi tu wala hayakufaa kuwa na kifaa cha kukinga silaha zingine kupenya,” akasema Bi Hussein.

Lakini wabunge wakiongozwa na mwenyekiti wao Opiyo Wandayi (mbunge wa Ugunja) walitaka kufahamu kulikuwa na haja gani kutumia Sh70,000 kwa kila vazi, wakai halikuwa na uwezo wa kukinga mtumizi kutokana na mavamizi yote.

Mbunge wa Tongaren Eseli Simiyu alisema kuwa mavazi hayo hayakuwa na ubora wa kutosha, akisema ni ya kutumiwa na raia, wala si polisi “ambao wakati mwingi wako katika hatari ya kulengwa kwa silaha.”

Idadi

Kulingana na ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa matumizi ya pesa za umma Edward Ouko, majaketi 600 ya aina hiyo yalinunuliwa bila vifaa hivyo vya kukinga watumizi kutokana na mavamizi ya silaha zingine.

Dkt Ouko alisema idara hiyo haikupata ubora uliofaa kutokana na pesa ilizotumia. Idara hiyo ilitumia jumla ya Sh43,272,500 kwa mavazi hayo.

Ilipokuwa ikinunua, idara hiyo ilisema mavazi hayo yalikuwa ya kutumiwa na askari wakati wowote wanapoitwa kusaidia katika utoaji wa huduma za usalama na asasi zingine za kiusalama, haswa wakati wa dharura.