Habari za Kitaifa

Mageuzi sekta ya kahawa yaibua maswali mengi

January 3rd, 2024 2 min read

NA JAMES MURIMI

SERIKALI inapojitahidi kuwakomboa wakulima wa kahawa kutoka mikononi mwa mabroka na wafanyabiashara walaghai, maswali yangalipo miongoni mwa Wakenya kuhusu mageuzi yanayoendeshwa katika sekta hiyo.

Mnamo Juni mwaka uliopita, moja ya maazimio yaliyopitishwa na wadau waliohudhuria Kongamano la Kahawa mjini Meru yalikuwa ni kufufuliwa upya kwa Chama cha Kitaifa cha Wakulima wa Kahawa nchini (New KPCU).

Kongamano hilo, ambalo lilikuwa limehudhuriwa na Naibu Rais Rigathi Gachagua, lilikubaliana kufufua sekta hiyo na kubaini changamoto zinazoikumba.

Serikali sasa imebaini New KPCU kama taasisi inayowaunganisha wakulima na wadau wengine katika sekta hiyo.

Chama hicho—ambacho kimekuwa kikisimamia sekta hiyo tangu miaka ya 1980—kinategemewa na serikali kama taasisi itakayolainisha sekta hiyo.

Kwa sasa, vyama vya ushirika vinawasilisha kahawa yake kwa New KPCU, ambacho baadaye husafirisha kahawa hiyo katika Soko Kuu la Kuuzia Kahawa la Nairobi (NCE).

Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Bw Timothy Mirugi, alisema kuwa limepewa nguvu na serikali, hivyo lina uwezo wa kusaga kahawa yote inayozalishwa nchini, kama lilivyokuwa likifanya miaka mingi iliyopita.

“Mnamo 1988, Kenya ilizalisha jumla ya tani 130,000 za kahawa, na KPCU ndilo lilikuwa shirika la pekee lililokuwa likisaga kahawa.

Uzalishaji sasa umepungua hadi tani 34,000 kwa mwaka. New KPCU bado inaweza kusaga kahawa hiyo, kwani ni chache ikilinganishwa na kiwango ilichosaga mnamo 1988. Tuna uwezo wa kusaga tani 16.5 kwa saa moja. Tuna nafasi ya kutosha ya kuhifadhi kahawa kwenye mabohari yetu,” akasema Bw Mirugi, kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Vyama vingi vya ushirika katika maeneo yanayokuza kahawa sasa vinategemea shirika hilo kuviuzia kahawa yao, hali ambayo imerejesha hadhi ya shirika hilo, kama ilivyokuwa hapo awali.

“Kwa sasa tuko kwenye msimu mpya wa kahawa ulioanza Oktoba. Tumefanya mauzo kadhaa na unaweza kuona dalili kwani bei zimeanza kupanda juu. Tumefikisha bei ya juu zaidi kwenye mauzo yetu—Sh340 kwa kilo moja. Hii ni ishara kwamba wanunuzi wameanza kuwa na imani nasi, wakulima wanapoendelea kutoa kahawa yao ili kuuzwa,” akasema.

Katika Soko Kuu la Kuuzia Kahawa jijini Nairobi, kuna maefu ya pakiti za kahawa kutoka viwanda tofauti vya kusagia kahawa nchini. Ni hali ambayo inawavutia wanunuzi tofauti, wanaopewa nafasi kuziangalia na kubaini ubora wake, kabla ya kuzinunua.

Kulingana na Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa NCE, Bi Lisper Ndung’u, kiwango cha uuzaji kimeimarika, hali ambayo imewavutia sana mabroka, ambao awali walikuwa wamesusia soko hilo.

“Kwa sasa tuna mabroka 14 wenye leseni za kuuzia kahawa. Hili ni ongezeko kubwa, ikizingatiwa kuwa mnamo Agosti 2022, kulikuwa na mabroka tisa pekee,” akasema Bi Ndung’u.