Habari

Magoha aagiza uchunguzi wa pili kisa cha unyama Nairobi School

July 10th, 2019 1 min read

Na JAMES MURIMI

WAZIRI wa Elimu Profesa George Magoha ameagiza uchunguzi ufanywe mara moja kuhusu madai ya kuwepo kwa visa vya wanafunzi kuwadhulumu wenzao Nairobi School na kuitisha ripoti katika kipindi cha wiki moja.

Waziri amesema anafahamu kuna uchunguzi mwingine unaondeshwa na maafisa katika wizara, lakini akaagiza usimamizi wa shule hiyo kumjuza binafsi matukio shuleni humo.

“Ninafahamu uchunguzi unaendelea, lakini ni muhimu zaidi kusikia kutoka kwa watu tuliowapa wajibu kusimamia watoto,” amesema Magoha.

Aidha amesema ana hamu kujua ni “nani alifanya nini na amechukuliwa hatua gani.”

Amesema hayo Jumatano asubuhi akiwa kwenye ziara ya ghafla katika Shule ya Msingi ya Nanyuki na DEB Nanyuki kujionea jinsi mtaala mpya wa kuzingatia uamilifu unavyoendeshwa katika shule hizo.

Shuleni Nairobi School, iliripotiwa kwamba mwanafunzi alijeruhiwa vibaya na viranja wa shule.

Shule nyingine ambayo kisa cha aina hiyo kimeripotiwa ni Savavongo School.