Magoha aapa kutetea CBC kwa hali na mali

Magoha aapa kutetea CBC kwa hali na mali

Na WINNIE ATIENO

WAZIRI wa Elimu, Prof George Magoha ameendelea kuutetea mfumo mpya wa Elimu unaoegemea kwa umilisi (CBC), na kwamba yuko tayari kuutetea hata kortini.

Prof Magoha alisema Jumanne kwamba mtaala huo wa CBC utaendelea licha ya kesi kuwasilishwa mahakamani kupinga utekelezwaji wake.

“Nipelekeni mahakamani mtanipata huko. Ninataka kuwahakikishia kuwa niko tayari kwa mapambano. Nitatetea mtaala huu kwa nguvu zangu zote,” akasema Prof Magoha kwenye hafla ya kuwatuza wanafunzi walioibuka bora nchini katika mashindano ya insha, Kaunti ya Kilifi.

Utata kuhusu mtaala huo mpya unaendelea nchini, na wiki jana wakili Esther Ang’awa alienda kortini kutaka CBC isimamishwe hadi kesi hiyo isikizwe na kuamuliwa.

Akiwa kama mmoja wa wazazi wanaoathiriwa na mtaala huo, Bi Ang’awa kupitia Rais wa Chama cha Mawakili (LSK), Nelson Havi, alisema serikali, kwa kutekeleza CBC, inakiuka haki za watoto kupata elimu.

“Ilani ya ombi hili pamoja na kesi hiyo kwa ujumla, vinaibua masuala mazito. Tunaamini yanafaa kuangaziwa na majaji wasiopungua watano, watakaoteuliwa na Jaji Mkuu,” akasema Bw Havi.

Lakini jana akiandamana na Waziri wa Utalii, Najib Balala, Prof Magoha alisema wizara yake imekuwa ikijizatiti kuhakikisha kuna usawa katika sekta ya elimu.

“Kenya si nchi tajiri Afrika lakini ndiyo inayotumia kiwango kikubwa cha fedha katika sekta ya elimu, ukiangalia bejeti yetu, sekta ya elimu inachukua asilimia 29 ya fedha,” alisema.

Hata hivyo, Prof Magoha aliungama kuwa kuna changamoto katika mtaala huo.

“Mjadala huu kuwa kama mzazi hajasoma hawezi kumsaidia mtoto wake hauingii akilini, mbona mamangu alinisaidia?” aliuliza.

Aliwataka wazazi wawe wabunifu katika masuala ya mtaala huo akisema wakitumwa kuleta mbolea kuna aina nyingi ikiwemo ile ya ng’ombe, kuku, na kadhalika.

Alisema mtaala wa awali wa 8-4-4 ulikuwa na changamoto kwani wanafunzi walilazimika kusomea mtihani badala ya kuwa wabunifu.

Prof Magoha pia aliwataka wazazi kuwasikiliza watoto wao ili waweze kujifikiria na kujieleza.

“Hatulazimishi mtu yeyote kuunga mkono mtaala huu lakini tuwe wakweli jamani. Mimi ni profesa na nina maoni yangu kuhusu elimu. Niacheni nifanye kazi yangu,” akasisitiza.

Bw Balala naye aliipongeza serikali kwa kutekeleza mtaala huo akisema wanafunzi wengiwe watatambua talanta zao mapema na kukuzwa.

Wakati huo huo chama cha wazazi nchini kiliwashtumu wanaopinga mtaala huo. Wazazi hao wanasema watashirikiana na taasisi za elimu nchini kuhakikisha CBC inafaulu.

“Sisi ndio wawakilishi wa zaidi ya wazazi milioni 10 nchini ambao wamewapeleka watoto wao kusomea shule za umma na hatujaongea wala kuishtaki serikali mahakamani. Tutajiungia na kesi hiyo kuelezea msimamo wetu katika swala la mtaala wa CBC,” alisema Bw Nicholas Maiyo mwenyekiti wa Chama cha wazazi nchini.

You can share this post!

NGILA: Teknolojia mpya ya mbegu sawa ila wapi hamasisho?

Vyombo vya habari vyatakiwa kuangazia habari za kilimo cha...