CECIL ODONGO na RUSHDIE OUDIA
ALIYEKUWA Waziri wa Elimu, Profesa George Magoha alikuwa ametoa ishara kuonyesha kwamba, alifahamu mapema siku ya kufa kwake ilikuwa imewadia.
Saa chache kabla ya kuaga dunia Jumanne, Prof Magoha aliagiza mkewe Dkt Barbara Odudu Magoha, kupigia simu mwanawe, Dkt Michael Magoha; mkaza mwana, pamoja na rafiki yake Dkt Walter Mwanda.
Kwa mujibu wa Dkt Mwanda, Prof Magoha aliyezimia mara nne kabla ya kukata roho dakika chache baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Nairobi, alifurahia kwamba muda wake wa kuondoka duniani ulikuwa umewadia.
Prof Magoha alifaa kusafiri jana Jumatano kuelekea Chuo Kikuu cha Maseno kuanza kazi ya kufundisha wanafunzi wanaosomea udaktari kabla ya kufariki akiwa na umri wa miaka 71.
Alipokuwa waziri, Bw Magoha alipendelea kuzungumzia maisha yake akisema kwamba angekuwa wa kwanza kufariki haswa alipohutubia vijana.
“Tunafaa kuhakikisha kuwa nchi yetu inakuwa bora. Hakuna atakayekuwa hai miaka 60 ijayo hapa ndani. Tutakuwa tumefariki sisi sote japo mimi nitakuwa miongoni mwa watakaokufa kwanza,” Prof Magoha alisema alipokuwa akihutubu kwenye mmojawapo wa mikutano.
Prof Magoha alifariki siku chache kabla ya kuanza shughuli ya kuandika kitabu cha kuelezea jinsi alivyoweza kudhibiti sekta ya elimu wakati wa janga la virusi vya corona mnamo 2020.
Shughuli hiyo ilifaa kuanza baada ya mazishi ya ndugu yake Profesa Alex Magoha aliyefariki akiwa nchini Amerika mwezi Desemba. Mazishi ya Alex yamepangwa kufanyika Jumamosi.
Hicho kilikuwa kitabu cha pili baada ya kingine kilichochapishwa mnamo 2017 kikielezea maisha yake kuanzia akiwa mvulana katika eneo la Gem, Kaunti ya Siaya, alipokuwa mwanafunzi katika Shule ya Upili ya Starehe na kisha masomo yake ya udaktari nchini Nigeria.
Kutokana na kifo hicho, kimya na huzuni jana ziliendelea kutanda vijiji vya Umiru, Yala na Ahono Ratudi eneobunge la Gem Kaunti ya Siaya anakotoka Profesa Magoha. Wanakijiji na majirani walimtaja kama kiongozi ambaye alileta mabadiliko makubwa, hasa katika sekta ya elimu.
Nyumbani kwa Profesa Magoha, kilomita moja kutoka barabara ya Kisumu-Busia, wafanyakazi wake walieleza Taifa Leo kuwa, walishangazwa na mauti ya mwajiri wao ambaye alikuwa akishughulika na mipango ya mazishi ya nduguye.
Walinzi na mfanyakazi wa nyumbani humo walilemewa na hisia huku wakisimulia nyakati za mwisho naye.
Saa chache kabla ya mauti yake, alikuwa amewapigia simu wafanyakazi na wanafamilia wake akiwemo dadake Pauline Dola, ambaye alikuwa ameelekea Kisumu kununua samani ya kuwekwa kwa nyumba ya Nyabera.
Mfanyakazi Gladys Akinyi ambaye amekuwa akisafisha nyumba ya waziri huyo wa zamani kwa muda wa miaka 20, alisimulia kuwa alizungumza na mwajiri wake siku ambayo alikufa.
Nyumbani kwa Bw Nyabera mita chache kutoka kwa boma la Profesa Magoha, kaburi lilikuwa likichimbwa pamoja na choo kando na maandalizi mengine.