NA DERICK LUVEGA
WALIMU wakuu watakaokiuka sheria inayowazuia kuwafukuza wanafunzi ambao hawajamaliza kulipa karo watakabiliwa na hatua ya kinidhamu ambayo haikufafanuliwa kuanzia wiki ijayo.
Haya yalisemwa Jumatano na Waziri wa Elimu Profesa George Magoha katika Kaunti ya Vihiga alipozindua rasmi madarasa ya CBC katika shule za sekondari za Simbi na Ingidi.
Profesa Magoha alisema mitihani ya kitaifa imesalia wiki mbili ianze na hakuna mtahiniwa yeyote anapaswa kuwa nyumbani kuhusiana na deni la karo ya shule.
Waziri alisema kuwa inasikitisha kuwa walimu wakuu kadhaa wanakiuka sheria inayolenga kuhakikisha wanafunzi hawafukuzwi shuleni kuhusiana na karo ambayo haijalipwa.
Alisema kuwa shule, wanafunzi na walimu ni mali ya serikali na wakati umewadia kuchukua hatua ya kutekeleza amri hiyo ambayo imekuwa ikikiukwa na baadhi ya walimu wakuu.
“Watoto wote ikiwemo walio na deni la karo ya shule ni sharti wabaki shuleni na kufanya mitihani ambayo imesalia wiki mbili ianze,” alisema Profesa Magoha.
“Tuna walimu wachache walio na ujasiri wa kutosha kuwafukuza wanafunzi kwenda nyumbani. Tunawahimiza wakome kwa sababu shule, walimu na wanafunzi wanamilikiwa na serikali.”
“Walimu wakuu hawana haki yoyote ya kuwafukuza watoto wakati wowote ambapo mitihani iliyolipiwa na serikali inaelekea kuanza. Wanapaswa kutulia na kuwahimiza wanafunzi wetu kutilia maanani mitihani. Watakaoendelea kukaidi watachukuliwa hatua ya kinidhamu kuanzia wiki ijayo,” alisema.
Onyo hilo limetolewa wakati kundi la maafisa wa Kuppet linalalamikia ucheleweshaji wa Wizara ya Elimu kutoa pesa za kufadhili kila mwanafunzi ikiwemo watahiniwa wa mitihani ya kitaifa.
Muungano huo umeshutumu mpango wa Wizara ya Elimu wa kushikilia fedha hizo hadi Aprili hatua inayodhamiriwa kupunguza kiasi cha fedha kilichotengewa wanafunzi wa Kidato cha Nne.
Profesa Magoha alitoa hakikisho kuwa madarasa 6,000 ya CBC yanayojengwa katika awamu hii ya kwanza yatakamilika kufikia Machi 7, wakati mitihani ya kitaifa imepangiwa kuanza.
Alisema madarasa 2,200 tayari yamekamilishwa na mengine 500 kuidhinishwa rasmi.
Waziri alisema kuwa Kaunti ya Garissa inaongoza ikiwa na asilimia 99 ya kukamilisha ujenzi wa madarasa hayo ikifuatiwa na kaunti za Meru na Mandera kwa asilimia 95 kila moja huku Wajir na Siaya zikiwa na asilimia 87.
“Tunatumai tutatimiza lengo letu. Kote nchini kiwango cha kukamilisha ujenzi kimefikia asilimia 72 ambapo asilimia 28 iliyosalia itakamilishwa kufikia Machi 7 kwa sababu ndipo mwisho wa muda uliotengewa awamu ya kwanza kwa kuwa shule zitakuwa zimeanza mitihani ya kitaifa,” alisema Profesa Magoha.
Alisema Wizara yake inakagua kila jengo ili kuhakikisha hakuna madarasa bandia.Waziri vilevile aliwakashifu wanasiasa wanaopigia debe kufutiliwa mbali kwa mfumo wa CBC na kusema kuwa mtaala huo tayari umeng’oa nanga na hautarudi nyuma. hivi punde utakuwa katika mwaka wake wa saba wa utekelezaji.