Magoha awataka wanahabari watathmini upya jinsi wanavyoangazia masuala ya elimu

Magoha awataka wanahabari watathmini upya jinsi wanavyoangazia masuala ya elimu

Na SAMMY WAWERU

WAZIRI wa Elimu Prof George Magoha amewataka wanahabari watathmini upya jinsi wanavyoangazia masuala ya sekta ya elimu badala ya kuiona serikali kama kwamba haijafanya maandalizi ya kutosha kipindi hiki ambacho wanafunzi wamerejea shuleni.

Shule zilifunguliwa rasmi mnamo Jumatatu, Januari 4, 2021, kote nchini, miezi tisa baada ya kufungwa kufuatia mlipuko wa janga la Covid-19.

Serikali imekosolewa kutokana na maandalizi yake duni kwa minajili ya ufunguzi wa shule, hasa kwa kutojenga madarasa ya kutosha katika shule za umma kusitiri idadi kubwa ya wanafunzi.

Baadhi ya shule za wamiliki binafsi zilizoshindwa kuafikia mahitaji ya ufunguzi kuzuia maenezi ya virusi vya corona zimefungwa, suala ambalo limechangia ongezeko la watoto katika shule za umma.

Mapema Jumatano, Prof Magoha alisema amekerwa na jinsi vyombo vya habari vilivyoikosoa serikali.

“Wanahabari wanafaa kuangazia masuala muhimu ya sekta ya elimu badala ya kutia zingatio katika kunipaka tope,” Prof Magoha amesema.

Siku kadha zilizopita, Prof Magoha alisema Kenya ni taifa kubwa na lisilopaswa kulinganishwa na mataifa mengine madogo katika ustawishaji wa maendeleo.

Waziri alitoa matamshi hayo yaliyozua mdahalo mkali kufuatia ulinganisho wa Kenya na Rwanda katika maandalizi ya ufunguzi wa shule, ambapo Rwanda chini ya kipindi cha muda wa mwaka mmoja pekee imetengeneza zaidi ya madarasa 22,000 ili kusaidia kuzuia maambukizi ya corona miongoni mwa watoto shuleni.

Naibu Waziri wa Elimu (CAS), Zack Kinuthia mnamo Jumanne katika ziara yake eneo la Pwani kutathmini jinsi shule zinavyoendelea kupokea wanafunzi, alinukuliwa akisema vyombo vya habari vimepigwa marufuku kuingia kwenye shule.

“Wanaopaswa kuwa shuleni ni wanafunzi na walimu pekee. Yeyote yule, wakiwemo waandishi wa habari wasiingie,” akaonya Bw Kinuthia.

Alisema wanaoingia shuleni kiholela wanahatarisha maisha ya wanafunzi, kwa kile alitaja kama “hawafahamiki iwapo wana virusi hatari vya corona au la”.

Alitetea amri hiyo akisema inalenga kuimarisha usalama wa watoto shuleni.

You can share this post!

Kaunti ya Mombasa yafuta kazi madaktari 86 akiwemo Chibanzi...

Natembeya awataka machifu Nakuru wawatafute na kuwarejesha...