Magoha azuia vyuo vikuu kuongeza karo, mageuzi

Magoha azuia vyuo vikuu kuongeza karo, mageuzi

Na FAITH NYAMAI

WAZIRI wa Elimu, Prof George Magoha amesitisha mipango ya vyuo vikuu kufanya mageuzi ambayo huenda yakasababisha maelfu kupoteza kazi.

Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN) wiki iliyopita kilitangaza kuwa kimepunguza idadi ya vitivo kutoka 35 hadi 11 na kuvunja baadhi ya idara kama hatua mojawapo ya kupunguza gharama ya kuendesha taasisi hiyo.

Chuo hicho pia kilifutilia mbali afisi tano za wasaidizi wa manaibu wa chansela na nyadhifa mbili za washirikishi wa naibu wa chansela.

UoN ni miongoni mwa mashirika na taasisi za serikali zinazolengwa kufanyiwa mageuzi ili kupunguza gharama.

Shirika la Kifedha la Kimataifa (IMF), mapema mwaka 2021, lilishauri Kenya kufanyia mabadiliko mashirika na taasisi zinazopata hasara kama moja ya masharti ya kupewa mkopo.

Lakini Prof Magoha alisema kuwa hakushauriwa na wala mageuzi hayo hayajachapishwa katika Gazeti Rasmi la Serikali.

Waziri Magoha, kupitia barua yake, iliyoandikwa Julai 14, kwa wakuu wa vyuo vikuu, anasema kuwa mapendekezo ya kufanya mageuzi ni sharti yapelekwe katika afisi yake.

Prof Magoha alisema Sheria ya Vyuo Vikuu ya 2012, inahitaji kwamba mapendekezo ya kufutilia mbali baadhi ya nyadhifa au kuvunja idara ni sharti yapelekwe kwa wizara ya Elimu ndani ya miezi mitatu baada ya kuidhinishwa na mabaraza ya vyuo vikuu.

“Barua hii ina mamlaka ya juu kuliko mawasiliano yote ambayo yametolewa hapo awali,” akasema Prof Magoha.

Kulingana na Sheria ya Vyuo Vikuu, wadhifa wa msaidizi wa naibu chansela na wakuu wa vitivo hauwezi kufutiliwa mbali bila idhini ya Mkuu wa Sheria na waziri.

You can share this post!

Wazee wa Kaya watakasa barabara

JAMVI: Ruto hatarini kupoteza chambo chake kisiasa