Habari Mseto

Magoha kuandaa kikao kujadili ratiba mpya ya shule

November 9th, 2020 2 min read

Na FAITH NYAMAI

WAZIRI wa Elimu, Prof George Magoha ameitisha mkutano wa wadau katika sekta ya elimu wiki hii kujadili kalenda mpya ya masomo shuleni, tarehe za mitihani ya kitaifa na namna ya kufidia miezi iliyopotea kutokana na janga la Corona.

Mkutano huo wa dharura, unalenga kujadili na kusuluhisha masuala ibuka kuhusu kalenda ya masomo baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza kuwa wanafunzi wa madarasa mengine watarejea shuleni Januari, 2021.

Wanafunzi wa gredi ya 4, Darasa la Nane na Kidato cha Nne walirejelea masomo ya kawaida mnamo Oktoba 5, 2020 chini ya uzingatiaji wa masharti ya kuzuia maambukizi ya Covid-19.

Ilitarajiwa kuwa wanafunzi wengine wangeripoti shuleni kuanzia Oktoba 26 hadi Novemba 6 lakini mipango hiyo ilisitishwa baada ya visa vya maambukizi ya corona, na vifo, kupanda zaidi ndani ya mwezi wa Oktoba.

Mkutano wa wiki hii pia unatarajiwa kujadili changamoto za kuwa na makundi mawili ya wanafunzi katika madarasa ya tano na kidato cha kwanza katika mwaka mmoja.

Suala hilo limeibuka kuwa gumu kutanzuliwa na walimu pekee bila kushirikishwa kwa wadau wengine.Kucheleweshwa kwa kurejelea masomo kwa wanafunzi wa shule za chekechea, wale wa gredi ya 1 hadi gredi 3, madarasa ya tano hadi saba na kidato cha kwanza hadi tatu kutokana na janga la corona kumeibua wasiwasi miongoni mwa walimu, wazazi na wanafunzi wenyewe.

Hii ni kutokana na muda ambao watakuwa wamepoteza wakiwa nyumbani.

Waziri Msaidizi wa Elimu, Zack Kinuthia aliambia Taifa Jumapili kwamba, wizara inajadili uwezekano wa kuunganisha kalenda ya mwaka ujao na wa mwaka huu ili kubuni mihula minne, badala ya tatu ilivyo kawaida.

“Tunaweza kuamua kuunganisha mihula ya pili na ya tatu kuhakikisha kuwa kalenda ya mwaka huu inatamatika kufikia Juni, 2021,” akaeleza.

Hii itapelekea kila muhula kudumu kwa miezi miwili na nusu pamoja na likizo ya wiki moja au mbili.Bw Kinuthia pia alisema wanatafakari kuhusu uwezekano wa kuchelewesha usajili wa wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa mwezi mmoja ili kuepuka uwezekano wa kuwa na makundi mawili ya wanafunzi katika kidato cha kwanza mwaka ujao.

Hii ina maana kuwa huenda wanafunzi watakaojiunga upya na kidato cha kwanza wakaripoti shuleni Julai, baada ya kundi la sasa kujiunga na kidato cha pili.