Habari Mseto

Magoha kung'atuka KNEC Machi 2019

December 22nd, 2018 1 min read

Na CHARLES WASONGA

MWENYEKITI wa Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC) Profesa George Magoha Ijumaa alidokeza kuwa kipindi chake kuhudumu katika baraza hilo kitakamilika Machi, 2019.

Akiongea wakati wa kutolewa kwa matokeo ya mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE) katika makoa makuu ya baraza hilo, Nairobi, alisema alikuwa akitoa hotuba yake ya mwisho kama mwenyekiti wake.

“Nimekuwa nikisema kuwa hakuna hali inayodumu… na miaka mitatu imekamilika. Kwa hivyo ikiwa Mungu alipanga kuwa hii itakuwa hotuba yangu ya mwisho, na iwe hivyo,” Profesa Magoha akasema.

Msomi huyo aliteuliwa katika wadhifa huo mnamo mwaka wa 2015.

Profesa Magoha alisema kuwa ikiwa muhula wake utakamilika mwaka ujao, sikitiko lake ni kwamba asasi hiyo bado haijaweza kupata afisi mpya katika mtaa wa South C. Vile vile, alisema KNEC haijaweza kujenga bohari nzuri ya kuhifadhi mitihani.

Profesa Magoha aliwashambulia wazazi ambao watoto wao hupatikana na hatia ya kushiriki wizi wa mitihani akisema wao (wazazi) ndio wanapasa kulaumiwa.

“Wazazi ndio hutoa pesa za kufanikisha udanganyifu katika mitihani. Mtoto huwa darasani.. hawangeenda nje kufanya maovu ambayo tumebaini walifanya. Wakosaji ni sisi wazazi na baadhi ya walimu waliopotoka kimadili,’ Profesa Magoha akaeleza.

Alisema KNEC ilihakikisha kuwa mitihani imelindwa akiongeza kuwa udangannyifu hutokea wakati wa kufirisha karatasi za mitihani kutoka kwa konteina kupelekwa shuleni.

Profesa Magoha ambaye zamani alikuwa Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Nairobi aliwashauri wazazi kukoma kununua karatasi feki za mitihani