Kimataifa

Magufuli amfuta kazi naibu waziri wa afya

May 17th, 2020 1 min read

Na THE CITIZEN

DAR ES SALAAM, TANZANIA

RAIS wa Tanzania John Pombe Magufuli amemteua Dkt Godwin Mollel awe Naibu Waziri wa Afya baada ya kumfuta kazi Dkt Faustine Ndugulile.

Kufutwa kazi kwa Dkt Ndugulile, 51, kumewashangaza wengi na kunafuatia mabadiliko mengine ambayo yalifanywa katika wizara hiyo majuma mawili yaliyopita.

Afisa huyo ambaye ni mtaalamu wa masuala ya afya ya umma amehudumu katika wizara hiyo kwa miaka mitatu.

Dkt Ndugulile aliteuliwa mnamo 2017 alipochukua nafasi ya Dkt Hamisi Kigwangala ambaye alipandishwa cheo na kuteuliwa Waziri wa Utalii na Maliasili.

Taarifa kutoka kitenngo cha mawasiliano cha Rais imesema kuwa naibu mpya wa waziri wa afya, Dkt Mollel alianza kuhudumu Jumamosi, Mei 16, 2020.

Mabadiliko haya yanajiri wakati ambapo ugonjwa wa Covid-19 unaathiri Tanzania na macho yote yanaelekezwa kwa Wizara ya Afya.

Tanzania imelaumiwa na mataifa jirani pamoja na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kwa kutoweka masharti ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa huo.

Mnamo Jumamosi Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta aliamuru kufungwa kwa mpaka wa nchi hiyo na Tanzania kufuatia ongezeko la visa vya maambukizi ya homa hiyo katika maeneo ya mpaka baina ya mataifa hayo mawili.

“Tumechukua hatua hii kuzuia visa vya maambukizi yanayotokana na wageni wanaoingia nchini,” akasema kwenye hotuba kwa taifa.

Hata hivyo, marufuku hayo yanasaza malori ya mizigo ambayo madereva na utingo wayo sharti wapimwe corona kabla ya kuruhusiwa nchini Kenya.

Kenya pia imezima watu kuingia na kutoka kupitia mpaka wake na Somalia kwa sababu zizo hizo.

Maelezo zaidi na CHARLES WASONGA