Kimataifa

Magufuli awaongoza Watanzania kumwomboleza Reginald Mengi

May 2nd, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

RAIS wa Tanzania John Magufuli Alhamisi aliwaongoza Watanzania na ulimwengu kwa jumla kuomboleza kifo cha mfanyabiashara bwanyenye Reginald Mengi ambaye alifariki Jumatano jioni akiwa na umri wa miaka 75 jijini Dubai.

“Nimepokea habari kuhusu kifo cha Mengi kwa huzuni kuu. Daima nitakumbuka mchango wake katika maendeleo nchini mwetu pamoja na maono yake aliyoyaandikia katika kitabu chake, ‘I can, I will, I must,” Rais Magufuli akaandikia katika akaunti yake ya Twitter. Kitabu hicho kitaanza kuuzwa madukani Julai mwaka huu.

Awali, vyombo vya habari vinavyomilikiwa na tajiri huyo ndivyo vilikuwa vya kwanza kutoa habari kuhusu kifo chake.

“Tunasikitika kutangaza kifo cha mwenyekiti mtendaji wa makundi ya kampuni kwa jina IPP Group of Companies. Dkt Reginald Mengi amefariki jijini Dubai Jumatano jioni,” gazeti la Tanzania, Guardian liliripoti katika tovuti yake.

Mengi alizaliwa mnamo 1944 katika familia maskini katika eneo la Kilimanjaro. Baadaye alianzisha shirika la habari lililohudumia Tanzania na maeneo mengine ya Afrika Mashariki likimiliki magazeti 11, redio na vituo vya televisheni, kulingana na jarida la Forbes.

Shirika hilo la habari pia linamiliki runinga za ITV, East Africa TV, Capital TV na redio za East Africa Radio, Radio One na Capital FM.

Pia ni mmiliki wa kampuni ya uchapishaji ya The Guardian Limited ambayo huchapisha magazeti ya “Guardian”, “Nipashe” na “Alaska”.

Vile vile, anamiliki kampuni za kutengeneza sabuni, kampuni ya kubwa ya kutayarisha maji ya chupa na soda nchini Tanzania. Vile vile, alijihusisha katika katika biashara ya uchimbaji madini ya dhahabu, uranium, shaba, chrome na makaa ya mawe.

Mnamo mwaka wa 2014, Dkt Mengi aliorodheshwa katika jarida la Forbes kama miongoni mwa watu tajiri zaidi barani Afrika. Baadaye aliondolewa katika orodha hiyo ambapo thamani ya utajiri wake ulikuwa dola 560 milioni (Sh56 bilioni).

Mengi pia anafahamika kama mhisani mkuu ambaye amelipia gharama ya matibabu kwa mamia ya watoto wenye maradhi ya moyo nchini India.

Kifo chake kimetokea miezi mitano baada yake kutangaza kuwa atawekeza katika sekta ya kutengeneza magari na uuzaji wa simu.

Mnamo Novemba mwaka 2018, Mengi alitia saini na kampuni moja ya Korea Kusini kuazisha kiwanda cha kutengeneza magari katika eneo la Kurasini kufikia Septemba 2019.

Kiini cha kifo chake hakijulikani, wala sababu ya  safari yake ya Dubai. Ameacha mke, Jacqueline Ntuyabaliwe, na watoto wanne.