Habari Mseto

Magufuli azungumza na Uhuru kumaliza uhasama maeneo ya mpakani

May 20th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI za Kenya na Uganda zimeingilia kati mgogoro unaohusu mipaka ya mataifa hayo ambayo ulikwamisha uchukuzi wa mizigo kwa siku kadhaa kuhusiana na janga la corona.

Mvutano huo uliendelea wiki hii kufuatia hatua ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kufunga mpaka wa Namanga na vijia vingine vya kuingia na kuondoka Tanzania kufuatia ongezeko la visa vya Covid-19 miongoni mwa madereva kutoka nchi hiyo jirani.

Saa chache baada ya Rais Kenyatta kutoa amri hiyo, zaidi ya madereva 20 wa malori ya masafa marefu kutoka Tanzania walizuiwa kuingia nchini Kenya baada ya kubainika kuwa na virusi vya corona.

Baada ya kisa hicho, mkuu wa mkoa wa Tanga Martin Shigella pia alipiga marufuku malori kutoka Kenya kuingia Tanzania, akidai madereva wa malori ndio huingiza virusi vya corona nchini humo.

Lakini Jumatano, Rais John Magufuli ametangaza kuwa amefanya mazungumzo na Rais Kenyatta na wakakubaliana mawaziri husika wa mataifa hayo mawili wasuluhishe mgogoro huo.

Akiongea alipozuru eneo la Singinda, Rais Magufuli amesema janga la Covid-19 halitasambaratisha uhusiana wa Tanzania na Kenya.

“Sisi ni majirani wema, nimeongea na Rais Kenyatta na tumekubaliana,” akauambia umati uliomshangilia.

“Tumekubaliana kuwa waziri wetu wa uchukuzi na mwenzake kutoka Kenya kwa ushirikiano na maafisa wa mipaka wa mataifa haya mawili waketi na kusuluhisha suala hili. Kenya na Tanzania ni mataifa ndugu,” akaongeza Rais Magufuli.

Kiongozi huyo amesema mataifa hayo ni washirika wa kibiashara na chumi zao zinategemeana.

“Chumi zetu zinapigana jeki, vitunguu vyetu huuzwa Kenya na Kenya hutuletea maziwa na bidhaa nyinginezo,” Rais Magufuli akaongeza.