Makala

Magugumaji na kemikali kero Ziwa Naivasha

March 24th, 2020 3 min read

NA RICHARD MAOSI

[email protected]

Kwa mbali utadhani ni sehemu mbili tofauti , yaani maji ndani ya ziwa Naivasha yaliyotenganishwa na uzuri wa mimea iliyosheheni rangi ya kijani kibichi karibu na ufuo.

Siku ya kawaida kama hii alfajiri na mapema Taifa Leo dijitali iliungana na mvuvi Peter Mwangi, mkaazi wa eneo la Kiragita Beach kaunti ndogo ya Naivasha kutalii mazingira ya ziwa Naivasha.

Akiwa amebeba nyavu, alituongoza katikakati ya kijia kilichotufikisha katika sehemu anayofanya kazi.

Tulisubiri kwa muda akitarajia kupokea samaki kutoka kwa wavuvi wenzake ambao wamekuwa wakimpokeza mzigo ili awauzie sokoni.

“Bei ya samaki mkubwa aliyekomaa ni baina ya 80 -100, lakini kwa sababu ya gharama ya usafiri waingiapo sokoni ni 150-200,”akasema , huku akichambua mzigo wake kwa makini asije akapunjwa.

Kinyume na siku za mbeleni anasema alikuwa akipokea takriban kilo 120 ya samaki kila siku, lakini siku hizi mambo yamebadilika, akijizatiti anaweza kupeleka sokoni kilo 30 hivi.

Mwangi anasema baadhi ya mambo yaliyosababaisha idadi ya samaki kupungua baharini ni kama vile magugu maji, mashamba ya maua na ndege wa mwitu hususan ndege wanaopenda kuwinda baharini mchana.

1.Magugu maji

Kero la magugu maji katika ziwa Naivasha ni hatari kwa ukuaji wa uchumi wa nchi , hususan kwa familia zinazotegemea uvuvi kama njia ya kukidhi mahitaji ya kila siku..

Kulingana na mwangi anasema tangu 2016 , wavuvi kutoka ziwa Naivasha wameshindwa kudhibiti ongezeko la kiwango cha magugu maji ndani ya ziwa.

Kwa upande mmoja analaumu serikali ya kaunti ya Nakuru na ile ya kitaifa, kwa kutotilia maanani nyenzo za kuangamiza magugu maji, jambo linalohatarisha viwanda vya samaki nchini.

Anasema kuwa magugu maji yalikuwa yamesambaa na kukwamisha usafiri ndani ya ziwa huku baadhi ya mashua za kufanyia uvuvi zikikwama ndani ya ziwa na kuhatarisha maisha ya wavuvi.

Kwa mfano mwanzoni mwa mwezi wa Machi watalii nane walikwama nadani ya ziwa Naivasha walipokuwa wakizuru sehemu ambayo ilikuwa imejaa viboko.

Nusura waangamie kama sio wavuvi wengine, walipoangana kuwaokoa na kuwapeleka katika hoteli yao wakiwa salama.

“Baadhi ya mashua zetu zimekwama na huwa inatulazimu kuitisha usaidizi kutoka usimamizi wa ziwa ingawa vifaa vya kufanyia uokozi ni haba,”akasema.

Wakati mmoja Taifa Leo Dijitali ilishuhudia baadhi ya wavuvi ambao wamekata tamaa baada ya kushindwa kuvuta boti zao kutoka kwenye magugu maji ambayo yalikuwa yamejaa hadi ufuoni.

Macharia anasema kuwa asilimia kubwa ya bahari imefunikwa na magugu maji, akiongezea kuwa hii ilikuwa ni hatari kwa wakazi wanaotegemea uvuvi hususan vijana wasiokuwa na ajira.

“Ingawa gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui alikuwa amewahakikishia wavuvi kuwa atatusaidia kukabiliana na magugu maji, bado anastahili kupiga marufuku uvuvi haram una uchafuzi wa maji ya ziwa,”alisema.

2.Uchafuzi wa maji ya ziwa kutoka kwa mashamba ya kukuza maua

Hatua chache kutoka hapo tunakutana na Bi Elizabeth Wanjira, ambaye anafanya kazi ya kuuza samaki kwa mikahawa ya wafanyibiashara mjini Naivasha.

Elizabeth alitufichulia kwamba maisha ya samaki katika ziwa Nakuru yalikuwa hatarini kwa sababu wamiliki wa mashamba ya maua, walikuwa wakipulizia mimea yao dawa nyingi kupita kiasi, ambazo hatimaye husombwa na maji hadi ndani ya ziwa.

Aliongezea kuwa hii ni hatari kwa ziwa Naivasha ambayo ndio ya kipekee inayotegemewa katika sehemu ya Mashariki ya Bonde la Ufa ijapo katika uvuvi.

Anasema kuwa idadi ya watu wanaokaa karibu na ziwa Naivasha ilikuwa imeongezeka sana kwa sababu ya upatikanaji wa ajira katika mashamba ya maua.

“Aidha wakati mwingine mitambo ya kupulizia dawa imekuwa ikifuja, na baadae Mafuta ya petrol yakaishia ndani ya ziwa na kuhatarisha Maisha ya samaki,”alisema Bi Elizabeth.

Msimu wa mvua imekuwa ukisafirisha dawa za kurashia kutoka kwenye mashamba ya wawekezaji wa kibinafsi wanaojihusisha na biashara ya maua hadi ndani ya ziwa jambo linalofanya wakati mwingine maji kubadilisha rangi.

Aidha ndege wanaokula samaki wamekuwa wakiangamia ishara tosha kuwa uchafuzi wa maji ndani ya ziwa Naivasha umekidhiri.

3.Ndege wa mwitu wasiokuwa na makazi

Ziwa Naivasha ni kivutio cha utalii kwa wageni wanaotoka mataifa ya mbali kujionea aina mbalimbali ya wanyama na ndege za kila sampuli.

Aina ya ndege kama vile pelicans, kingfisher, na mwewe wanapenda kutafuna samaki aina ya tilapia ambao wamejaa katika ziwa Naivasha.

Elizabeth aliongezea kuwa ndege aina ya mwewe wana uwezo mzuri wa kuona hadi ndani ya maji na wanaweza kunyaka samaki kwa haraka na kupaa kabla ya kufikiwa na wavuvi.

Wakati mwingine ndege wamekuwa wakiwapokonya wavuvi samaki wakiwa baharini , ama wakawaandama wavuvi hadi ufuoni kuwapokonya samaki.

Mapendekezo

Mtaalam wa samaki katika Chuo Kikuu cha Eldoret Dkt Elizabeth Mwikali anasema ni wakati raia wajifundishe jinsi ya kukuza samaki katika mazingira yao ya kibinafsi kwa njia ya vidimbwi.

Hii ni kwa sababu ya ongezeko la uchafuzi wa maji , unaoambatana na maradhi sugu hasa pale binadamu wanapokula samaki ambao wameadhirika.

Mwikali aliongezea kuwa samaki wanaofugwa ndani ya vidimbwi mara nyingi hulishwa vyema na maji huwa ni safi na salama.

Aidha mayai ya samaki huwa ni salama kiasi kwamba hayawezi kusombwa na maji hasa mvua kali inapokuja