Habari Mseto

Magunia 11 ya bangi yanaswa, mlanguzi ahepa

September 12th, 2018 1 min read

NA RICHARD MAOSI

POLISI katika eneo la Naivasha Jumatatu usiku walishambulia nyumba ya mlanguzi wa dawa za kulevya na kunasa magunia 11 na misokoto 80 ya bangi. Bidhaa hiyo haramu ilikuwa ya thamani ya Sh2 milioni.

Taarifa kutoka kwa wakazi wa eneo la Kayole, karibu na mji wa Naivasha walitoa habari hizo kwa polisi walioandama makazi yao saa 11.00 usiku na kufanikiwa katika oparesheni yao. Mmiliki wa nyumba hiyo ambaye ni mwanamke alibahatika kutoroka.

Naibu afisa mkuu kutoka Naivasha Bw John Kwasa alieleza kuwa mwanamke huyo amekuwa akihusika na vitendo vya uhalifu katika miji mikuu humu nchini.

”Tunafahamu huwa anaendesha biashara zake katika maeneo ya Kiambu, Naivasha na Nairobi lakini bado tumejizatiti katika juhudi za kumtia mbaroni hivi karibuni,” alisema.

Bw Kwasa alieleza kuwa biashara hii imemwezesha mwanamke huyo kujistawisha japo sio kazi halali.

Pia wamezidisha juhudi kusaka wahusika wanaomsaidia kusafirisha na kuuza mihadarati’. “Ni kundi la wahalifu wanaoendesha kazi hii na bila shaka tutahakikisha tunawakamata, ” alisema.

Bw Kwasa aliwahimiza wakazi kushirikiana na polisi kuzima ulanguzi wa mihadarati akisifia kitendo hiki cha kuwapasha askari.