Makala

MAGWIJI WA WIKI: Nyota wa KCPE 2019

November 20th, 2019 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

WENGI wa wanafunzi waliowahi kutawazwa washindi wa mikumbo mbalimbali ya Shindano la Uandishi wa Insha na kushirikishwa na shule zao katika mradi wa Newspapers in Education (NiE) unaoendeshwa na gazeti la Taifa Leo, walijizolea alama bora zaidi katika somo la Kiswahili katika mtihani wa KCPE 2019.

Kupitia NiE, kampuni ya Nation Media Group (NMG) inatumia Taifa Leo kuimarisha na kuboresha viwango vya kusomwa na kufundishwa kwa Kiswahili na masomo mengine katika shule za mingi na upili za humu nchini.

Dylan Ingala aliyeibuka mshindi wa mkumbo wa Mei 2019 kutoka The Ideal School Kitengela, alikwangura jumla ya alama 427 baada ya kupata alama 92 katika Kiswahili.

The Ideal School Kitengela katika Kaunti ya Kajiado, ni miongoni mwa shule nyingi ambazo kwa sasa zinatambua umuhimu wa NiE, mradi unaozidi kuwa tupa ya kipekee ya kuwatia makali wanafunzi wanaojiandaa kwa mitihani ya kitaifa.

Zaidi ya Ingala, wengine waliotia fora zaidi shuleni humo ni Noel Muita aliyezoa jumla ya alama 405 na 91 katika Kiswahili na Tacy Daniela aliyejizolea alama 404 na 89 katika Kiswahili.

Shule nyingine iliyotia fora zaidi ni ya Precious Site iliyoibuka bora katika kaunti nzima ya Kiambu baada ya kusajili alama wastani ya 392.30.

Kati ya wanafunzi waliofaulu vyema zaidi katika shule hii ni Bridget Wangui (422), John Kiaro (418), Gabriel Maina (418) na Evanson Githumbi (418). Flavian Onyango aliyeibuka miongoni mwa wanafunzi bora katika orodha ya watahiniwa waliotia fora zaidi kwenye ngazi ya kitaifa, alizoa jumla ya alama 439 baada ya kupata 98 katika Kiswahili. Mwanafunzi huyo wa St Teresa Chakol Girls Boarding, Busia alishiriki Hamasisho la NiE kikamilifu mwanzoni mwa Aprili 2019.

Akidumisha umahiri wake katika lugha, Shantal Mkagakwaya Ndegwa wa Riara Group of Schools, Nairobi alizoa jumla ya alama 434 na 96 katika Kiswahili. Aliibuka mshindi wa Insha za Taifa Leo katika mkumbo wa Machi.

Isaac Kamau Magu wa Tender Care Junior Academy, Nairobi alijizolea alama 97 katika Kiswahili na jumla ya 425, matokeo ambayo kwa mujibu wa mwalimu wake Djibril Nyangweso, ni ya kuridhisha sana, ya kutia moyo na ya kuonewa fahari.

Griffin Arama Matundura wa Elsa Preparatory Academy, Kisii alizoa alama 91 katika Kiswahili na jumla ya 434, tatu nyuma ya Fabiola Mukabane wa Booker Academy, Mumias aliyekwangura alama 95 katika Kiswahili.

Ayub Osman kutoka Kinderworld Academy, Nairobi alipata jumla ya alama 419 na kuibuka wa kwanza shuleni humo baada ya kuzoa alama 89 katika Kiswahili. Wengine waliofaulu vyema katika shule hiyo ni Aisha Ayni (415), Ayub Ahmed (409) na Asia Hassan (402).

Duran Joseph Otieno wa Twin Kids Academy, Nairobi alipata alama 77 katika Kiswahili na jumla ya 400 huku Boniface Wesonga Odhiambo wa Shule ya Msingi ya Alung’oli, Busia akizoa jumla ya alama 426 na 91 katika Kiswahili. Roman Salapei Lemeyian na Erica Ouma Anyango wa St James Saika Campus, Nairobi walijizolea jumla ya alama 412 kila mmoja na alama 92 na 90 katika Kiswahili mtawalia.

Emmanuel Efedha wa Saphire Academy, Vihiga aliyeibuka mshindi wa Februari, alikwangura alama 92 katika Kiswahili na jumla ya 415. Mwenzake Aljamal Aziz aliyeshinda Agosti alizoa alama 89 katika Kiswahili na jumla ya 404, sita nyuma ya Ivy Embosani aliyepata 91 katika Kiswahili. Drogba Atemu aliibuka mwanafunzi bora shuleni Saphire Academy kwa jumla ya alama 428 na 98 katika Kiswahili.

Latasha Ndirangu Wairimu wa Rockfields Junior School, Nairobi aliibuka mshindi wa mkumbo wa Oktoba.

Alizoa alama 94 katika KCPE Kiswahili na jumla ya 424.

Latasha Ndirangu Wairimu kutoka Rockfields Junior School, Nairobi aliyezoa alama 94 katika Kiswahili huku akipata jumla ya alama 422 katika KCPE 2019. Picha/ Hisani

Audrey Wachera, Teyanna Beth na Lynette Chelangat waliibuka wanafunzi bora zaidi shuleni humo baada ya kupata jumla ya alama 427 kila mmoja.

Olivia Moraa Moibi aliibuka mshindi wa mkumbo wa Aprili katika Shindano la Insha za Taifa Leo. Mwanafunzi huyu wa Corradini Catholic, Nairobi alizoa alama 89 katika Kiswahili na jumla ya 424. Wengine waliopata alama za juu shuleni humo ni Shaleen Twily (412), John Griffin (406) na Anthony Thumbi (404).

Katika Shule ya Msingi ya Pen Elite Githunguri, Kiambu wanafunzi Trina Wangui (427), Morris Njenga (427), Hellen Atieno (426), Abraham Muchiri (425), Kindness Mukami (421) na Eunice Kagunyi (421) ndio waliotia fora zaidi.

Mnamo Agosti 2016, Shule ya Msingi ya Carmelvale Academy, Nairobi ilimtoa mwanafunzi Lucy Wangari Njuguna aliyejizolea jumla ya Sh50,000 za karo baada ya kuibuka mshindi katika mkumbo wa mwisho wa Shindano la Uandishi wa Insha za Taifa Leo.

Mnamo 2017, wanafunzi Loice Mitchele wa Saphire Academy (Vihiga), Douglas Ngumo Wacera wa Utafiti Academy (Kiambu) na Abdulbasit Abdullahi Sheikh wa California Academy (Nairobi) walijizolea jumla ya Sh50,000 za karo kila mmoja katika Kitengo cha Shule za Msingi.

Gikambi Faraja Precious wa Utafiti Academy (Kiambu), Sarah Nasambu (Kitale School) na Rehema Nemuel (Qubaa Muslim School) ndio waliotawala Shindano Kuu la Kitaifa mwaka 2018.

Shindano Kuu la mwaka 2019 litafanyika Novemba 28, 2019, katika vituo vifuatavyo: Nairobi, Mombasa, Kisumu, Kakamega, Eldoret, Nyeri na Kitui.