MAGWIJI WA WIKI: The Munenes

MAGWIJI WA WIKI: The Munenes

MAURINE Nyawira Munene ni mke wa Dennis Munene Kabiru ambaye pia ni mhubiri na mwimbaji stadi wa nyimbo za injili.

Walifunga pingu za maisha Juni 2019 baada ya kuchumbiana kwa takriban miaka sita na wamejaliwa mtoto – Majesty Mwega – aliyezaliwa Juni 2021.

Ingawa walikulia katika vijiji tofauti vya Kaunti ya Kirinyaga, Maurine na Dennis almaarufu The Munenes, walishiriki kanisa moja na wakajiunga na kundi la ‘Big Family’ walilotumia kueneza Ukristo na kukuza maadili miongoni mwa vijana wenzao.

Mbali na kukoleza penzi baina yao, kundi hilo liliwanoa zaidi kisanaa na wakawa maarufu miongoni mwa waumini wa Kanisa la Christian Worship International Ministry Kirinyaga kati ya 2010 na 2014.

Maurine Nyawira Munene (kushoto) akiwa na mume wake ambaye ni Dennis Munene Kabiru. PICHA | CHRIS ADUNGO

Tangu waanze safari yao ya muziki pamoja, wanandoa hawa wameachilia vibao vinne wanavyopania kujumuisha na nyimbo nne watakazochomoa mwisho wa wiki ijayo kisha kuhifadhi katika albamu.

‘Niguse’ ni kazi ya kwanza waliyoitoa Desemba 2020 kabla ya kufyatua wimbo ‘Wa Ajabu’ uliotamalaki tuzo za kifahari za E360 Awards jijini Nairobi mwaka wa 2022.

Walicharaza kibao ‘Haujawahi Shindwa’ mnamo Julai 2022, miezi mitano baada ya kuachilia ‘Hallelujah’.

Kubwa zaidi katika maazimio yao kisanaa ni kuendelea kutoa kazi zinazokubalika kimataifa huku wakichomoa kibao kipya kila baada ya miezi mitatu.

Matamanio yao mengine ni kushirikiana kikazi na wasanii wengi ndani na nje ya Afrika Mashariki ili kutumia uimbaji kuipa jamii mwelekeo.

The Munenes watarekodi vibao vinne vipya katika ukumbi wa Nairobi Cinema mnamo Januari 28, 2023.

Mbili kati ya nyimbo hizo zitashirikisha mwimbaji maarufu kutoka Kenya, Evelyn Wanjiru, na msanii mzoefu raia wa Tanzania, Dkt Ipyana Peter Kibona.

Hafla hiyo ya Worship Experience & Live Recording inatazamiwa kuvutia maelfu ya watu na itanogeshwa pia na baadhi ya waimbaji wabobevu wa nyimbo za injili kutoka pembe mbalimbali za dunia.

The Munenes waliteuliwa kuwa wahubiri katika Kanisa la Revival Times Chapel jijini Nairobi mnamo Aprili 2022.

Zaidi ya kushauri wanandoa wachanga, wanategemewa pakubwa kuwaelekeza vijana kimaadili, jinsi ya kujikuza kisanaa na namna ya kujitegemea na kukabili changamoto mbalimbali maishani.

“Fahamu unachokitaka na utambue unakokwenda. Kipende unachokifanya na jinsi unavyokifanya. Shindana na wakati. Weka Mungu mbele, jitume na uombe sana,” wanashauri.

Maurine alilelewa katika kijiji cha Kamugunda, Kirinyaga.

Ndiye mwanambee katika familia ya watoto watatu wa Bw Duncan Muchiri na Bi Margaret Wakuthii. Alisomea katika shule ya msingi ya Miracle Academy, Kirinyaga, kabla ya kujiunga na Kagumo Girls High, Kirinyaga (2011-2014). Ana diploma ya masuala ya usimamizi biashara (Banking & Finance) kutoka Thika College of Banking & Accountancy (2016-2018).

Aliwahi kuwa mhasibu msaidizi katika kampuni ya Cookiko Ltd mjini Ruiru (2018-2019).

Maurine Nyawira Munene (kushoto) akiwa na mume wake ambaye ni Dennis Munene Kabiru. PICHA | CHRIS ADUNGO

Dennis alitekwa na kipaji cha uimbaji katika umri mdogo na akajitungia zaidi ya nyimbo 10 katika kidato cha pili. Alianza safari ya elimu katika shule ya msingi ya Kiambatha, Kirinyaga (2002-2009) kabla ya kujiunga na Mutige Boys High, Kirinyaga (2010-2013) kisha kusomea uanahabari katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya (2014-2016).

Aliwahi kuhudumu katika duka la Tuskys mjini Thika (2017-2018) kabla ya kuwa msimamizi wa masuala ya mauzo katika kampuni ya Excellent Choice Investment Ltd.

Alilelewa katika kijiji cha Mutaga, Kirinyaga na ndiye wa pili kuzaliwa katika familia ya watoto watatu wa Bw Evanson Kabiru Njeru na Bi Rose Karimi.

Maurine Nyawira Munene (kulia) akiwa na mume wake ambaye ni Dennis Munene Kabiru. PICHA | CHRIS ADUNGO
  • Tags

You can share this post!

Kaunti ya Mombasa yatangaza kuanzisha mradi wa fedha za wadi

KINYUA KING’ORI: Ni haki ya kila Mkenya popote...

T L