Habari Mseto

Mahabusu 10,000 waachiliwa kipindi cha corona

September 30th, 2020 1 min read

MARY WAMBUI na CHARLES WASONGA

ZAIDI ya wafungwa 10,000 wenye makosa madogo wameachiliwa huru kutoka magereza mbalimbali nchini wakati wa janga la Covid-19, Kamishna wa Magereza Wycliffe Ogallo amethibitisha.

Hatua hii inapelekea magereza 129 kote nchini kusalia na wafungwa 42,596.

Kuachiliwa huru kwa wafungwa hao ni sehemu ya mapendekezo yaliyowasilishwa na Baraza la Kitaifa la Kusimamia Haki (NCAJ) kwa lengo la kupunguza misongamano katika magereza ya humu nchini.

Waliochiliwa huru ni wafungwa waliokuwa wakutumikia kifungo cha chini ya miezi sita au wale ambao walibakisha miezi sita kukamilisha kifungo chao.

Mnamo Aprili mwenyekiti wa NCAJ, Jaji Mkuu David Maraga alitangaza kuwa Mahakama Kuu ilianza kupokea faili za wafungwa wa makosa madogo kuzikagua kabla ya kuwaachilia huru.

Shughuli hiyo ilipelekea wafungwa 4,800 kuachiliwa huru wakati huo kama hatua ya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Hatua zingine ambazo Idara ya Magereza Nchini ilichukua kupambana na janga hili ni kuanzishwa kwa vituo vya kutenga wafungwa wanaoshukiwa kuambukizwa virusi hivyo na kusikizwa kwa kesi za wafungwa kwa njia ya mtandao.