Habari Mseto

Mahabusu apatikana na corona jela la Manyani

June 14th, 2020 1 min read

NA LUCY MKANYIKA

Mfungwa mmoja ametengwa katika kituo cha afya cha Rekeke katika Kaunti ya Taita Taveta baada ya kupatikana na virusi vya corona.

Mfungwa huyo kutoka jela la Manyani alipelekwa kwenye kituo cha afya Jumamosi usiku baada ya wenzake waliotangamana kupelekwa karantini.

Duru zilisema kwamba mahabusu huyo alikuwa ametolewa kwenye jela la Shimo la Tewa.

Maafisa wa kaunti wa kushughulikia dharura wameanzisha kutafuta waliokuwa wametangamana na mgonjwa huyo huku serikali ikishughulika kupambana na virusi hivyo.

Waziri wa Afya wa kaunti hiyoJohn Mwakima alisema kwamba wanaendelea kutafuta habari zaidi.

“Walikuwa wawili lakini mmoja amepelekwa karantini.”

Jumamosi serikali iliwaachilia wagonjwa wengine tisa huku waliopona virusi hivi wakifika 15 katika kaunti ya Taita -Taveta.

Kaunti hiyo pia imeanza kupima kwa wingi wafanyabiashra wanaoishi katika barabara kuu ya Nairobi kuelekea Mombasa.