Habari

Mahabusu asimulia kortini alivyopelekwa benki na polisi kutoa Sh200,000 za hongo

March 14th, 2018 1 min read

Na KITAVI MUTUA

MSHUKIWA wa wizi alishangaza mahakama moja Kaunti ya Machakos Jumatano, kwa kudai kwamba alitolewa seli za polisi na kusindikizwa hadi benki kutoa Sh200,000 alizowahonga maafisa wakuu wa polisi ili wamwachilie huru.

Jacob Mutinda Kilonzo, mmoja wa washukiwa waliovamia boma la mfanyabiashara mjini Matuu na kupiga kambi kwa wiki moja wakila na kustarehe wiki iliyopita, alilaumu polisi kwa kukosa kutatua kesi nje ya mahakama baada ya kupokea hongo.

Mshukiwa huyo alisimulia Hakimu Mkuu Mkazi wa Kithimani Gilbert Shikwe jinsi alivyokubaliana na mkuu wa kituo cha polisi cha Matuu (OCS), Richard Okudoyi, na naibu wake watatue kesi hiyo kabla ya kufika kortini baada ya kulipa hongo.

“Nilisindikizwa kutoka kituo cha polisi hadi tawi la Matuu la benki ya Kenya Commercial na kurudishwa seli baada ya kutoa Sh200,000 ambazo zilipaswa kugawanywa kati ya maafisa wa polisi na mlalamishi ili niachiliwe huru,” mshukiwa alieleza mahakama.

Tawi la Matuu la benki ya Kenya Commercial. Picha/ Hisani

Risiti

Ili kuthibitisha madai yake, Bw Kilonzo aliwasilisha risiti ya benki kuonyesha kwamba alitoa pesa benki mnamo Alhamisi, Machi 8, saa tisa na dakika hamsini na tisa, dakika moja kabla ya benki kufungwa.

Kulingana na kitabu cha matukio katika kituo hicho, mshukiwa alikamatwa Jumatano Machi 7 na kusajiliwa chini ya nambari OB3/8/3/2018, saa nane usiku. Kwa hivyo, alikuwa kizuizini wakati pesa zilipotolewa benki kulingana na risiti aliyowasilisha kortini.

Bw Kilonzo alishangaza mahakama kwa kuinua mikono na kuomba asaidiwe kupata pesa zake akisema kwa kumfungulia mashtaka ya wizi, polisi hawakutimiza ahadi yao ya kumwachilia baada ya kuwapa hongo.

Mama yake, Loise Mutinda, ambaye pia alikuwa kortini aliunga mkono madai ya mwanawe.