Habari Mseto

Mahabusu waliotoroka wakanusha shtaka

July 8th, 2019 2 min read

Na Richard Munguti

MAHABUSU wawili kati ya 17 waliotoroka wameshtakiwa Jumatatu. Washukiwa hao walitoroka wakiwa wanarudishwa katika gereza la Viwandani wakitoka mahakama ya Thika.

Amos Wanyoike Wanjiru na James Kamau Wanjiru, walifikishwa mbele ya Hakimu Mwandamizi, Bi Martha Mutuku ambapo walikanusha shtaka la kutoroka walipokuwa chini ya ulinzi wa askari jela wanne, Koplo Paul Nangiro, Konstebo Michael Njuguna, Konstebo John Macharia na Konstebo Zacharia Maroa Keya.

Upande wa mashtaka unaoongozwa na wakili wa Serikali, Bi Pamela Avedi ulipinga washukiwa hao kuachiliwa kwa dhamana.

“Napinga washukiwa hawa wawili kuachiliwa kwa dhamana. Walikuwa miongoni mwa washukiwa 17 waliotoroka kutoka kwenye lori la idara ya magereza katika eneo la Muthurwa kaunti ya Nairobi,” alisema Bi Avedi.

Mahakama ilijulishwa kuwa washukiwa hao walitoroka walipokuwa wanarudishwa gerezani.

“Kulikuwa na msongamano mkali wa magari washukiwa walipotoroka,” alisema kiongozi wa mashtaka.

Bi Avedi aliomba afisa anayechunguza kesi hiyo aruhusiwe kuwasilisha ushahidi wa kuandikwa ikisimulia jinsi washukiwa hao wa wizi wa mabavu walivyotoroka walipokuwa wakirudishwa rumande kutoka mahakama ya Thika mnamo Julai 3, 2019.

Washtakiwa hao walitoroka kwa kukata vyuma vilivyochomelewa. Mahakama ilijulishwa kuwa polisi wanaendelea kuwasaka washukiwa wengine waliochana mbuga.

“Naomba kesi hii itajwe baada ya wiki mbili kuwezesha mahakama kuripoti kuhusu uchunguzi unaoendelea kuwasaka washukiwa waliotoroka,” alisema Bi Avedi.

Mahakama iliamuru washukiwa hao wazuiliwe gerezani kabla ya kesi inayowakabili kutengewa siku ya kusikizwa.

Wakati huo huo, kusikizwa kwa kesi inayowakabili maafisa wanne wa polisi wa utawala na kachero iliahirishwa baada ya wakili Cliff Ombeta kutofika kortini kwa madai ya kuwa anaugua.

Maafisa hao wa usalama wamekanusha kumuua wakili Willy Kimani, mteja wake Josephat Mwenda na dereva wa teksi Joseph Muiruri.

Ushahidi muhimu ulikuwa umeorodheshwa kutolewa jinsi mmoja wa washukiwa hao alivyoungama jinsi Kimani, Mwenda na Muiruri walivyouawa baada ya kutekwa nyara wakitoka mahakama ya Mavoko iliyoko mjini Athi River, kaunti ya Machakos.

Mashahidi 30 wameorodheshwa kutoa ushahidi. Polisi wa utawala walioshtakiwa ni Fredrick Leliman, Stephen Cheburet, Sylvia Wanjiku na Leonard Maina Mwangi.

Kachero aliyeshtakiwa pamoja nao ni Peter Ngugi. Wamekanusha mashtaka matatu ya mauaji mbele ya Jaji Jessie Lesiit.