Habari Mseto

Mahakama kuamua iwapo itazuru bwawa la Patel

July 18th, 2018 1 min read

NA PETER MBURU

Mahakama ya kutatua mizozo ya mashamba na mazingira Nakuru imesema kuwa itaamua ikiwa itazuru eneo la mkasa wa bwawa la Solai, kama sehemu ya kesi iliyoko mbele yake.

Mahakama hiyo ilisema hivyo Jumanne baada ya kualikwa na mawakili wa mwakilishi wa wodi ya Kabazi Dkt Peter Mbae, ambaye ameshtaki mamlaka za NEMA, WARMA na wamiliki wa shamba la Patel ambapo bwawa lake lilichangia vifo vya watu 48.

Mawakali Bernard Kipkoech Ngetich, Gordon Ogola na Robert Owino wanaitaka mahakama hiyo kuzuru eneo la mkasa ili ipate ufahamu wa uzito wa suala hilo, baada ya kujionea hasara lililosababisha bwawa hilo.

Hii ni baada ya Dkt Mbae kufikisha kesi hiyo mbele ya Jaji Dalmas Ohungo mnamo Juni 19, akiitaka mahakama kusimamia shughuli ya kufanya ukaguzi wa kimazingira na ubora wa mabwawa yaliyo katika mashamba ya Patel kwa afya ya binadamu.

“Tunaalika korti kufanya ziara katika eneo la mkasa ili masuala yatakayosemwa mbele yake tyaibue taswira halisia, baada yao kujionea uzito wa suala hilo,” akasema wakili Ngetich.

Bw Ohungo aidha alizitaka pande zote zilizoshtakiwa pamoja na zingine ambazo zingetaka kuhusishwa katika kesi hiyo kuwasilisha majibu yao ndani ya siku 14.

Korti sasa itatoa uamuzi ikiwa itazuru eneo la Solai mnamo Novemba 15, Jaji Ohungo akasema.

Katika kesi hiyo, Dkt Mbae anaitaka mahakama kuongoza shughuli za ukaguzi wa ubora wa mabwawa ya Patel, kisha uamuzi wake utumiwe kutafutia waadhiriwa wa mkasa wa Mei 9 ridhaa.

Aidha, Dkt Mbae anaitaka mahakama kuamuru wamiliki wa shamba la Patel kurekebisha mazingira na kurejesha mikondo ya maji ya mito waliyofungia katika hali yake ya jadi.

Muungano wa mawakili nchini, LSK umejumuishwa kwenye kesi hiyo.

“Kwa kuzingatia hali yake ya sasa, kuna hitaji la dharura ukaguzi wa ubora wa kimazingira na hali ya afya wa mabwawa kwenye shamba la Patel ili kuzuia mikasa siku za usoni,” karatasi za kesi hiyo zinasema.