Mahakama kuu yazima makadhi

Mahakama kuu yazima makadhi

NA PHILIP MUYANGA

MAHAKAMA Kuu imeamua kuwa mahakama za kadhi hazina mamlaka ya kusikiliza na kuamua kesi zinazohusu masuala ya ustawi wa watoto.

Mahakama hiyo iliongeza kuwa, katiba na sheria kuhusu mahakama za kadhi ziko wazi kuwa mamlaka ya masuala yanayohusu watoto yamekabidhiwa Mahakama ya Watoto.

Katika uamuzi wa rufaa iliyowasilishwa dhidi ya uamuzi wa Kadhi aliyeagiza mwanamume kulipa karo ya shule, gharama ya matibabu na mahitaji mengine ya watoto, Jaji Reuben Nyakundi alisema kuwa katiba ina mipaka iliyoweka dhidi ya mamlaka ya mahakama ya kadhi kusikiza na kuamua kesi za watoto.

Jaji Nyakundi alisema hakuna mamlaka kwa mahakama ya kadhi kushughulikia madai yanayohusiana na ustawi wa watoto, kwa kigezo cha makubaliano, ukaribu, urahisi au mazingira yasiyo ya kawaida.

Alisema rufaa ya mume huyo aliyetajwa katika stakabadhi za mahakama kama MNO ilikuwa imefaulu kwani mahakama ya kadhi ilitekeleza mamlaka ambayo haikuwa nayo au yasiyopatikana katika katiba.

“Nakubaliana na wakili wa mlalamishi katika rufaa hii kwamba kushughulikia masuala ya malipo au maagizo yoyote kuhusiana na ustawi wa watoto kuhusu ndoa hiyo kunatokana na mamlaka ambayo hayapo na ni makosa,” alisema Jaji Nyakundi.

Aliongeza kuwa mambo muhimu yaliyotiliwa mkazo kuhusiana na masuala hayo hayakufaa kushughulikiwa na mahakama ya kadhi.

Katika mahakama ya kadhi, SJM ambaye ni mwanamke, alikuwa ameshtaki MNO akitaka talaka ambayo alipewa mbali na haki zake kama zilivyo chini ya sheria ya Kiislamu.

Kati ya haki ambazo mwanamke huyo alitaka, mahakama iliambiwa ni gharama ya kutunzwa kwa watoto na gharama ya kutunzwa kwake yeye mwenyewe.

Mahakama hiyo ya kadhi pia ilimkubalia kuishi na watoto na kuamuru MNO kumlipa mwanamke huyo thuluthi tatu ya mshahara wake au Sh13,000 kila mwezi au kilicho zaidi kati ya hali hizo mbili.

Katika rufaa yake ya kupinga uamuzi huo, MNO alisema mahakama ya kadhi ilikosea kisheria kwa kuamua masuala ya watoto na gharama ya utunzaji wao bila kuwa na mamlaka.

Alisema mahakama ya kadhi ilikosea kisheria kwa kukosa kutilia maanani uwezo wake wa kifedha ikilinganishwa na majukumu ya kifedha aliyopewa na pia kuangalia masuala ambayo hayakuwa muhimu bila ushahidi yaliyofanya kutelekezwa kwa haki.

MNO pia alisema Kadhi alikosea kisheria kwa kukataa ushahidi wake bila sababu yoyote ya kisheria au mamlaka.

Jaji Nyakundi pia aliongeza kusema kuwa tofauti na Mahakama ya Hakimu, mamlaka ya mahakama ya kadhi huwa ni madogo.

You can share this post!

Vilio Koome aingilie kati kesi za kupinga ufufuzi wa Mumias

Mbunge apokea baraka za maaskofu

T L