Habari

Mahakama ya juu yasema ina mamlaka ya kusikiliza kesi ya magavana

October 8th, 2019 1 min read

Na BENSON MATHEKA

MAGAVANA walipata ushindi katika Mahakama ya Juu, majaji walipoamua kwamba wana mamlaka ya kusikiliza kesi iliyowasilishwa na Baraza la Magavana (COG) kuhusu mzozo wa kiwango cha pesa ambacho serikali za kaunti zinapaswa kutengewa.

Baraza la Magavana liliwasilisha kesi likitaka ufafanuzi wa kisheria kuhusu jinsi serikali za kaunti zinapaswa kutengewa pesa na mfumo unaopaswa kutumiwa.

Hata hivyo,bunge ambayo ni miongoni mwa washtakiwa katika kesi hiyo, ilitaka kesi hiyo kutupiliwa mbali ikisema Mahakama ya Juu haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Kulingana na Spika wa bunge Justin Muturi, Mahakama ya Juu haikufaa kusikiliza kesi ya magavana kwa sababu kuna kesi nyingine kuhusu suala hilo katika Mahakama Kuu.

Kwenye uamuzi uliosomwa na Jaji Njoki Ndung’u jana, majaji walitupilia mbali ombi la bunge la taifa kwamba halina mamlaka ya kusikiliza na kuamua kesi hiyo.

Alisema kesi hiyo inahusu maslahi ya umma na inafaa kusikilizwa na kuamuliwa.

Hata hivyo, Jaji Ndung’u alifafanua kuwa ingawa mahakama hiyo ina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, haitashughulikia masuala yote ambayo Baraza la Magavana iliwasilisha katika kesi yake.

Kulingana na Jaji Ndung’u, majaji wataeleza masuala watakayoshughulikia Oktoba 16 mwaka huu.

Kesi hiyo ilitokana na mzozo kati ya Bunge la Taifa na Seneti kuhusu mswada wa ugavi wa mapato wa 2019 ambapo maseneta walitaka kaunti zitengewe Sh335 bilioni lakini wabunge wakazipunguza hadi Sh316.5 bilioni.

Mzozo huo ulitishia kulemaza huduma katika serikali za kaunti kamati ya upatanishi ya seneti na bunge iliposhindwa kufikia muafaka kuhusu suala hilo.

Maseneta walikubali pesa zilizotengewa serikali za kaunti lakini wakasema hawangeondoa kesi katika mahakama ya juu.