Habari Mseto

Mahakama ya Milimani yafungwa siku 14

July 30th, 2020 1 min read

Na BENSON MATHEKA

MAHAKAMA ya Milimani iliyo jijini Nairobi, ambayo ndiyo kubwa zaidi nchini, itafungwa kwa siku 14 kuanzia leo Alhamisi baada ya maambukizi ya virusi vya corona kuripotiwa humo.

Jaji Mkuu David Maraga alisema Jumatano mahakama hiyo ilifungwa baada ya wafanyakazi kadhaa kuonyesha dalili za ugonjwa wa Covid-19 katika kipindi cha wiki moja iliyopita.

Alisema mfanyakazi mmoja alithibishwa kuambukizwa virusi vya corona.

“Mfanyakazi huyo alikuwa ametangamana na wenzake kadhaa kabla ya kuthibitishwa alikuwa na corona. Uongozi wa Mahakama kwa kushauriana na wakuu wa Mahakama ya Milimani na maafisa wa wizara ya afya, umeamua kusimamisha shughuli katika mahakama hiyo ili kuwezesha wafanyakazi wote kujiweka karantini na baadaye kupimwa kabla ya kurudi kazini,” Bw Maraga alisema kwenye taarifa.

Alieleza kuwa, Mahakama ya Milimani itafungwa kwa siku 14 kuanzia leo.

Katika kipindi hicho, kesi za dharura zitashughulikiwa kupitia mtandao. Jaji maraga aliagiza wakuu wa vitengo tofauti kuweka mikakati ya kushughulikia kesi hizo.

Kuna zaidi ya korti 100 katika mahakama ya Milimani ambayo huwa inahudumia maelfu ya watu kila siku.

Wiki iliyopita, mahakama ya Makadara iliyoko Mashariki mwa jiji pia ilifungwa kwa siku 14 baada ya wafanyakazi wawili kuambukizwa virusi vya corona.

Mahakama ya Mombasa ilikuwa ya kwanza kufungwa mwezi jana baada ya wafanyakazi kadhaa kuambukizwa virusi hivyo.