Habari Mseto

Mahakama ya Rufaa yabatilisha uamuzi kuhusu wahandisi 115 wa KQ

August 22nd, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

KAMPUNI ya Ndege ya Kenya Airways imeshinda kesi ambapo Mahakama ya Rufaa imetoa uamuzi kuwa ilikuwa makosa kurejeshwa kazini kwa wahandisi 115.

Mahakama hiyo ilisema agizo la Jaji Hellen Wasilwa, la kuwarejesha kazini kwa muda wahudumu hao halikuwa na msingi kwa sababu wafanyikazi hao hawakuthibitisha sababu maalum za kurejeshwa.

Majaji William Ouko, Kathurima M’Inoti na Fatuma Sichale walikubaliana na wakili wa KQ Githu Muigai kwamba Bi Wasilwa alifanya uamuzi peke yake bila ushahidi wa kitaalam kuhusiana na usalama wa safari za ndege.

Joseph Otieno Oyuga na 114 walifika mahakamani Desemba 2017 baada ya kampuni hiyo kuwafuta kazi wahandisi na mafundi waliokuwa wamegoma kwa kusema mgomo huo ulikuwa haramu.

Wafanyikazi hao walipuuza notisi tatu za kurejea kazini. Mafundi walikuwa wakiitisha nyongeza ya asilimia 70, ilhali wahandisi walikuwa wakiitisha nyongeza ya asilimia 250.