Kimataifa

Mahakama yaagiza kijana ahame kwao ajitegemee

May 23rd, 2018 1 min read

VALENTINE OBARA Na MASHIRIKA

NEW YORK, AMERIKA

WAZAZI wameshtaki mtoto wao wa kiume mwenye umri wa miaka 30, wakitaka mahakama imwamuru kuhama kwao ili ajianzishie maisha.

Shirika la habari la CNN liliripoti kuwa wazazi hao walikuwa wamempa mwanao, Michael Rotondo ilani mara tano ahame na hata wakajitolea kumlipia kodi ya nyumba atakayohamia lakini wapi! Akakwamia kwao kama kupe.

Kwa kujitetea, kijana huyo alisema alifaa kupewa ilani miezi sita kabla siku ambapo alihitajika kuhama.

“Nilitaka tu kupewa muda wa kutosha kabla nihame, ikizingatiwa kuwa wakati nilipopewa ilani hizo sikuwa na uwezo wa kujitegemea,” CNN ilimnukuu kusema.

Wazazi wake, Christina na Mark Rotondo wanaoishi Camillus, waliwasilisha kesi mahakamani mapema mwezi huu wakaonyesha mahkama ilani walizomkabidhi mwanao kuanzia Februari hadi Machi mwaka huu.

“Kufikia sasa tumeona hujaonyesha nia yoyote ya kujiandaa kuhama. Tunakuonya kuwa tutachukua hatua yoyote iwezekanayo kuhakikisha umehama kama ulivyoagizwa,” sehemu ya ilani hizo inasema, kwa mujibu wa mashirika ya habari.

Jaji Donald Greenwood alikubaliana na wazazi wake na kuagiza ahame mara moja kwani alipewa muda wa kutosha kujipanga, lakini kijana huyo akasema atakata rufaa.

Kijana huyo asiye na ajira alidai kuwa kwa miaka minane tangu aliporudi nyumbani, hakuna siku ambapo aliambiwa achangie kwa mahitaji ya nyumbani wala kusaidia kwa kazi za nyumbani au ukarabati wa nyumba kwa hivyo kesi hiyo ilikuwa na nia mbaya.