Habari Mseto

Mahakama yaagiza Miguna aachiliwe mara moja

March 27th, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Kuu Jumanne iliamuru wakili Miguna Miguna anayezuiliwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) tangu Jumatatu usiku aachiliwe mara moja.

Na wakati huo huo Jaji Roselyn Aburili alimwagiza Dkt Miguna afike kortini Jumatano.

Jaji Aburili alitoa maagizo hayo baada ya kusikiza kesi iliyowasilishwa na mawakili John Khaminwa, Nelson Havi na Julie Soweto.

Mawakili hao waliomba mahakama iamuru Dkt Miguna aachiliwe pasipo na masharti yoyote.

Mawakili hao waliofika katika uwanja wa JKIA pamoja na James Orengo na Cliff Ombeta Jumatatu kumlaki waliiomba mahakama iamuru Dkt Miguna aruhusiwe na idara ya Uhamiaji kuingia nchini pasipo na vikwazo vyovyote.

Baada ya kusikiza mawasilisho na tetezi za mawakili hao , Jaji Aburilili aliamuru Dkt Miguna aachiliwe mara pasi na masharti.

Dkt Miguna amewashtaki Waziri wa Usalama  Dkt Fred Matiang’i, Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji  mshtakiwa Gordon Kihalangwa, Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) Joseph Boinnet na Mkurugenzi wa Idara ya Jinai George Kinoti.

Pia kamanda wa Polisi JKIA na Mwanasheria Mkuu wameshtakiwa.

Katika ushahidi uliowasilishwa kortini , mawakili hao walisema Dkt Miguna amezuiliwa katika Choo katika uwanja wa JKIA na kwamba Pasi yake ya kusafiria ya nchi ya Canada imetwaliwa.

Jaji Aburili alifahamishwa kwamba washtakiwa wanaomzuilia Dkt Miguna walikaidi maagizo ya mahakama mwezi uliopita walipotakiwa kumfikisha kortini na badala yake wakamsafirisha hadi nchini Canada kwa madai ni raia wa nchi hiyo.

Jaji alifahamishwa washtakiwa walikuwa wameagizwa na Jaji Enoch Mwita wamtayarishie Dkt Miguna hati za kurudi kwake nchini.

Pia walikuwa wameamriwa wahakikishe mwanasheria huyo asumbuliwi akiwa huku nchini. Jaji Mwita alisema katika uamuzi wake kwamba Dkt Miguna ni mzaliwa na raia wa Kenya aliyehamia Canada.

“Mlalamishi anahisi kwamba atadhulumiwa na kuteswa na hatimaye kufurushwa kutoka humu nchini kinyume cha haki zake,” alisema Bw Havi.

Jaji alifahamishwa zaidi: “Pasi yake ya kusafiria imetwaliwa tayari ikiwa ni hatua ya kutaka kumtangaza mtu asiye na kwao.”