Mahakama yaagiza mwanamume, 52, arudishiwe mahari baada ya talaka

Mahakama yaagiza mwanamume, 52, arudishiwe mahari baada ya talaka

NA GERALD BWISA

MWANAMUME mwenye umri wa miaka 52 hatimaye amerejeshewa mahari na wakwe zake baada ya mahakama ya Kitale kukubaliana na ombi lake.

Mahakama iliagiza Bw Wilberforce Saenyi Murunga arudishiwe ng’ombe watatu, mbuzi mmoja na Sh20,000 alizotoa kwa wazazi wa aliyekuwa mke wake.

Mifugo hao watarejeshwa nyumbani kwake katika kijiji cha Chwele, Kaunti ya Bungoma, wikendi hii.

Watapokelewa na wazee wa ukoo wake wa Balunda.

Bw Murunga alitoa mahari ya Sh50,000, ng’ombe wanne, mbuzi mmoja, viatu na kofia mnamo Aprili 27, 2019, huko Bungoma.

Lakini Bw Murunga aliafikiana na wakwe zake kuwa atawaachia ng’ombe mmoja, Sh30,000, viatu na kofia.

“Nimefurahi kwamba mahakama imenitendea haki. Nilidhani kesi hii ingetupiliwa mbali kwa sababu mkwe wangu niliyemshtaki ni wakili. Nashukuru Mungu nimeshinda,” akasema Bw Murunga.

Alieleza kuwa kurejeshwa kwa mahari hiyo ni ishara kwamba mke wake huyo wa zamani yuko huru.

Bw Murunga aliachana na mkewe Irine Khasoa kutokana na kigezo kwamba alitoroka nyumbani na kwenda kuishi kwingine. Wawili hao walitalakiana rasmi Oktoba 12, 2021 katika mahakama ya Kitale.

Katika stakabadhi zilizowasilishwa kortini mnamo Desemba 2021, Bw Murunga alisema mkewe alitoroka nyumbani baada ya kuishi naye kwa mwaka mmoja na miezi sita pekee.

Aprili 14 mwaka huu, mahakama hiyo ya Kitale iliagiza pande zote mbili kufika mbele ya mpatanishi wa korti.

Bw Murunga alieleza kwamba ilikuwa haki yake kurejeshewa mahari kwani aliwakilisha maelfu ya wanaume wanaoumia kimyakimya.

Alihimiza wanaume kwenda kortini kutafuta haki badala ya kuumia pasipo kuchukua hatua.

  • Tags

You can share this post!

Wanjigi achagua wakili mwaniaji mwenza

Kalonzo atatiza kampeni za Sonko kwa kuhepa Raila

T L