Makala

Mahakama yaamua muratina si pombe haramu

February 24th, 2024 3 min read

NA MWANGI MUIRURI

WATU wengi katika jamii ya Agikuyu sasa wanasherehekea uamuzi wa Mahakama Kuu kwamba pombe aina ya Muratina si haramu na inaweza ikaandaliwa na kubugiwa pasipo na hofu ya kukamatwa na polisi ama maafisa wa serikali za kaunti almaarufu kanjo.

Pombe hiyo huandaliwa kupitia mkorogo wa maji yaliyochanganywa na sukari ya miwa pamoja na asali.

Kisha matunda yaliyovunwa kwa mti unaofahamika kama sausage tree ambao kitaaluma kabisa hufahamika kama Kigelia africana, hutumbukizwa ndani ya mchanganyiko huo na mkorogo huo kufunikwa na kuachwa uive katika mazingara ya joto la kadri.

Matunda hayo ya mti wa sausage tree kwa lugha ya Gikuyu hufahamika kama miratina hivyo basi kuipa pombe hiyo jina la muratina.

Katika uamuzi uliotolewa na Jaji Abigail Mshila wa Mahakama ya Kiambu, pombe hiyo ambayo hutumika katika hafla za kitamaduni, nyingi zikiwa sherehe za ulipaji mahari na ufungaji wa pingu za maisha katika harusi, ni maarufu kiasi kwamba watunzi wa nyimbo za kimila huitambua na kuiweka kwa hadhi ya juu sana kimila.

Utawasikia wazee katika hafla hizo wakisema “na uheshimu muratina kwa kuwa ndio pombe iliyotumika kumpoza mamangu” huku hata waliookoka katika imani za kukemea pombe wakishurutishwa kuibugia wakikabidhiwa kwa amri ‘takatifu’ kwamba “ukipewa ya mtoto (bi harusi) huwezi ukaimwaga”.

Ingawa vijana wa sasa humimina pombe hiyo kwa vikombe, mikebe na sahani, kitamaduni na kiasili kabisa, ni pembe za ng’ombe ndizo hutumika kuibugia.

Aidha, vizazi vya siku hizi hubugia muratina kusaka ulevi lakini kitamaduni muratina ni kinywaji cha kubariki na kutakasa ili kudumisha amani na wavyele.

Hakuna mzee wa kitamaduni anayeweza kubugia muratina bila kwanza kumwaga kidogo ardhini kwa ‘wavyele’ hao wanaosemwa ni roho za waliokufa kitambo kwa jina, ngomi.

Katika siku za hivi karibuni, maafisa wa usalama wamekuwa wakiandama wote wanaoandaa muratina bila idhini ya machifu.

Akitoa uamuzi wake, Jaji Mshila alisema kwamba “kwa sasa kinachohitajika ni baraza la wazee la Kiama Kia Ma kushirikiana na idara ya utawala ili kuwe na mikakati ya kuhakikisha muratina inabugiwa katika hafla za kitamaduni kwa mikakati ambayo haikaidi sheria za nchi.

Mfadhili wa baraza la Kiama Kia Ma Kung’u Muigai ambaye ni binamuye Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, alisema kwamba uamuzi huo ni wa kipekee kwa kuwa umedumisha msimamo wa jadi wa jamii ya Agikuyu.

“Ni jukumu letu katika jamii sasa kulinda nembo hiyo yetu kupitia kukataa harakati zote za kudunisha pombe hiyo. Tunajua kumekuwa na wakora ambao huiandaa kwa msingi wa kibiashara na katika harakati za kufanya iwe kali zaidi, wanaongeza bidhaa nyingine kama pombe kali pamoja na mihadarati,” akasema Bw Muigai.

Aliongeza kwamba wazee ndio watakuwa na wajibu wa kulinda ‘utakatifu’ wa muratina kupitia kuhakikisha inaadaliwa katika nyakati za hafla za kitamaduni, zikishirikisha wanaofaa, katika mazingara safi na kwa nidhamu za kudhibiti ulevi kiholela.

Aliyekuwa mbunge wa Naivasha John Mututho alisema “muratina inaweza ikaandaliwa kama bidhaa ya kibiashra bora tuwe na leseni ya kibiashara”.

“Ni lazima muratina ipite katika kila awamu ya viwango vya ubora vilivyowekwa,” akasema Bw Mututho.

Alisema jamii ya Agikuyu inaweza ikaandaa muratina kwa msingi wa kuvutia pesa za watalii na pia wateja wa kibinafsi.

Mwenyekiti wa baraza la Agikuyu Wachira Kiago alisema hakuna jipya katika uamuzi huo kwa kuwa “sisi kama washirikishi wa utamaduni wetu tunatambua muratina kama kiungo thabiti na cha kuenziwa katika jamii ya Agikuyu”.

Bw Kiago alisema hata haelewi ni kwa nini kulikuwa na walioenda kortini kusaka idhini ya muratina katika tamaduni za Agikuyu kwa kuwa “kwa vyovyote vile na linginepo lile, muratina iko sawa katika jamii na pengine tu Mungu wetu atukanye kutumia kinywaji cha aina hii”.

Kinara wa Narc-Kenya Martha Karua aliteta kwamba “tumekuwa tukishuhudia udhalimu wa vitengo vya serikali kujaribu kuzima jamii kujumuika pamoja kutekeleza wito wa kitamaduni kwa msingi hafifu wa kupambana na magenge”.

Alisema kwamba mfano ni tukio la Desemba 31, 2023, ambapo wazee wa kati ya umri wa miaka 66 na 90 walikamatwa katika Kaunti ya Murang’a wakisingiziwa kuwa wafuasi wa genge haramu la Mungiki.

[email protected]